Friday, July 17, 2015

CHADEMA WAMPOKEA LOWASSA


Lowassa ChademaMbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa (ndani ya gari) akilakiwa na makada wa CHADEMA alipowasili mkoani Arusha juzi jumatano.
Na Sifael Paul
Mamia ya makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha, wamejitokeza kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa (pichani) ambaye ni mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Juzi Jumatano, habari zilizopatikana kutoka kwa mtoa taarifa wetu jimboni humo zilieleza kuwa, wanachama hao walifikia hatua hiyo kufuatia jina la Lowassa kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kupitia chama chake, nafasi ambayo ilichukuliwa na Dk. John Pombe Magufuli.
ANAKWENDA KUJIANDIKISHA
Baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba Lowassa angeenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kijijini kwake, Ngarash, Monduli ndipo wanachama hao wa chama hicho kikuu cha upinzani walipokusanyika barabarani wakimsubiri.
“Watu walikuwa ni wengi sana. Ukweli walikuwa ni mamia. Kuna walioweka kambi nyumbani kwake kumsubiri (alikuwa akitokea jijini Dar). Walikuja kumpokea kwa shangwe. Kila mtu alikuwa na bendera ya Chadema.
“Wengi wa wanachama wa Chadema wanaojiita makamanda walikuwa ni bodaboda ambao kila mmoja alikuwa amechomeka bendera ya Chadema kwenye pikipiki yake, kichwani walikuwa wamevaa boshori (aina ya kofia) za Chadema. “Wakati mzee (Lowassa) anajiandikisha, zoezi ambalo kwa sasa linaendelea mkoani humo, nje ya kituo hicho, wanachama wa Chadema walipaza sauti, wakiimba ‘mzee karibu Chadema’, karibu CDM, wewe ni jembe, jiwe walilolikataa waashi litakuwa jiwe kuu la pembeni’ huku wakimalizia na people’s…power,” alisema mtoa habari wa gazeti hili na kuongeza:
“Walikuwa wakimwambia Lowassa kuwa Mwalimu Julius Nyerere hakukosea aliposema kuwa upinzani wa kweli utatoka CCM hivyo wakati ndiyo huu. Ilibidi kuimarisha ulinzi hadi Lowassa amalize kujiandikisha kwani kwa kadiri muda ulivyokuwa ukisonga ndivyo watu walikuwa wakiongezeka.”
WATAKA TAMKO LAKE
Mtoa habari wetu alieleza kwamba, baada ya Lowassa kujiandikisha, alipotoka nje ili kuondoka eneo hilo kuelekea nyumbani kwake, wanachama hao walimzingira wakitaka kusikia tamko lake, wakimuomba kujiunga na Chadema.
Alisema kuwa Lowassa aliingia kwenye gari tayari kuondoka eneo hilo na msafara wake lakini makada hao waliziba barabara kwa pikipiki wakimuomba aseme neno juu ya kuhamia Chadema ambacho wanaimani nacho ili roho zao zitulie.
NENO LA LOWASSA
Hata hivyo, Lowassa ambaye hakutaka kuzungumza chochote huku akionekana mwenye huzuni, alivunja ukimya ili wamwachie aende zake akawaambia.
“Endeleeni kuwa na imani na chama chenu (Chadema).”
Baada ya kusema maneno hayo, Lowassa aliondoka kuelekea nyumbani kwake huku wanachama hao wakimsindikiza, wakiimba people’s power.
DURU ZA KISIASA
Ukiachilia mbali tukio hilo lililovuta hisia za wengi, duru za kisiasa ziliyaangazia madai kwamba, wanachama hao hawakukurupuka kwani madai ya Lowassa kuhamia Chadema yalikuwa yameenea kilakona ya nchi.
Mara tu baada ya kukatwa kwa jina lake mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kurejea jijini Dar, ilidaiwa kwamba alifanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema juu ya kuhamia kwenye chama hicho na kupata nafasi ya kugombea urais ili akapimane ubavu na Dk. John Magufuli.
ZOEZI LA KUHAMIA CHADEMA
Habari za kina zilidai kwamba, zoezi hilo la Lowassa kukihama chama chake ambacho amekuwa kada wake kwa miaka 38 na kwenda Chadema lilikwamishwa kwa namna mbili.
Mosi; ilidaiwa kuwa makubaliano yake na Chadema hayakwenda sawia kwani viongozi hao wa juu wa Chadema hawakuafikiana.
Pili; duru za kisiasa zilieleza kuwa Lowassa alikutana na wazee wa CCM ambao walimweleza madhara ya kukihama chama hicho na mustakabali wake wa baadaye kisiasa.
MTU WA KARIBU
Akizungumzia suala hilo la tishio la kuhamia Chadema, mmoja wa watu wake wa karibu (jina tunalo) aliliambia gazeti hili kuwa, watu wasubiri muda ukifika Lowassa atautangazie umma uamuzi wake.
KINGUNGE ASISITIZA
Wakati upepo ukiwa bado haujatulia, kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru ameendelea kusisitiza kwamba Lowassa ndiye chaguo sahihi la chama hicho kwa ngazi ya urais kwani kitendo cha kuliengua jina hilo kimeacha kasoro na mpasuko ndani ya chama chake.
Alisema kuwa, licha ya jina lake kutopitishwa kugombea urais badala yake akapitishwa Dk. Magufuli bado anaamini yeye ndiye mshindi katika sakata hilo kwa kuwa ndiye mgombea anayependwa zaidi na WatanzaniaLove to hear what you think!