Wednesday, June 17, 2015

MSIMU WA TANO WA AIRTEL RISING STARS WAZINDULIWA LEO

Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo akipiga mpira kuashiria kuzinduliwa kwa michuano hiyo.
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana Tanzania, Ayoub Nyenzi, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano na Rais wa TFF, Jamal Malinzi baada ya kuzinduliwa kwa michuano hiyo.
Wachezaji walioibuliwa kwenye michuano hiyo ambao kwa sasa wapo na kikosi cha timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, kutoka kushoto ni Sherida Boniface, Stumai Abdallah, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Maimuna Hamis, Najihath Abas, Neema Paul na Amina Ally.
Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waliokuwepo kwenye uzinduzi huo.
 MSIMU wa tano wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 inayojulikana kama Airtel Rising Stars, umezinduliwa leo katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel, Kinondoni Morocco jijini Dar.
Michuano ya mwaka huu inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 8 katika mikoa tofauti ikiwa ni hatua ya awali huku ile ya fainali ikifanyika Septemba 11 mpaka 21 jijini Dar ambapo itazishirikisha timu za wanaume za mikoa ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Mbeya, Mwanza na Morogoro na za wanawake ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya na Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema kampuni yao ina nia thabiti ya kusaidia maendeleo ya soka hapa nchini huku wakijivunia mafanikio waliyoyapata kwenye misimu minne iliyopita.
Katika hatua nyingine, Singano alitangaza kampuni hiyo kuingia mkataba na kiungo wa Ivory Coast na Klabu ya Manchester City, Yaya Toure kwenye kampeni yao ya It’s Now yenye lengo la kulea na kukuza vipaji barani Afrika kupitia nyanja mbalimbali za michezo.
Naye mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo, alisema serikali inatambua michuano hiyo kuwa kipaumbele kwenye kuinua soka letu huku Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akiupongeza mpango huo wa kukuza soka la vijana kwani ndiyo msingi wa maendeleo ya soka letu

Wednesday, June 3, 2015

Urais 2015: Wassira atinga makao Makuu CCM kuchukua fomu ya Urais


Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira akikabidhiwa fomu ya kugombea urais.
 

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira akishuka kwenye Gari ili kuchukua fomu ya kugombea urais 2015 .
 

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira akiwasili ukumbini katika mkutano na Waandishi wa Habari leo.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira akisaini wakati wa kuchukua fomu ya kugombea urais paembeni ni mke wake.
 
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira leo amekabidhiwa fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama  cha Mapinduzi huku kipaumbele chake kikubwa  kikiwa ni  kuinua kilimo.
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari hivi sasa  katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu Wassira  amesema  ikiwa atachaguliwa kuwa rais ataboresha kilimo kwa kutumia zana za kisasa huku akisisitiza kuwa  jembe la mkono litawekwa katika vyumba ya makumbusho ili iwe historia.
 
Kwa upande wa ufisdi amesema ufisadi ni wizi,anausikia tu na kwa sababu atakuwa rais atahakikisha kuwa anawachukulia sheria pamoja na kuziongea nguvu sheria ili kupambana nao.
 
Akizungumzia Muungano amesema atatetea na kuulinda maana kuuvunja ni kugawa nchi.

BLATTER AJIUZULU FIFA


Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter.
Zurich, Uswis
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter, jana alijiuzulu cheo chake kutokana na kashfa ya rushwa iliyolikumba shirikisho hilo.Blatter alitangaza kujiuzulu jana jioni zikiwa ni siku nne tangu alipochaguliwa kwa mara ya tano kuiongoza Fifa.
Alitangaza uamuzi huo kwenye makao makuu wa Fifa mjini Zurich akiwa ametumikia cheo cha urais kwenye shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka 17.
“Nimekuwa nikijituma sana kwa kipindi changu chote nilichokaa kwenye taasisi hii kubwa duniani, maisha yangu ni soka na ninaupenda sana mchezo huu.“Nilikuwa nataka kufanya kila kitu kizuri kwenye taasisi hii kubwa, lakini labda sasa niseme kuwa nimeamua kujizulu wadhifa wangu wa urais wa Fifa kutokana na kashfa hii ya rushwa ambayo imetukumba.
“Nataka kuwashukuru wale wote waliokuwa wananiunga mkono kwa kipindi chote ambacho nilikuwa rais wa Fifa, lakini pia natakiwa kuwashukuru wale ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha soka linakuwa,” alisema Blatter.
Kwa takribani wiki sasa, Fifa imekuwa ikilaumiwa na wadau mbalimbali baada ya kuibuliwa kwa tuhuma za rushwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) zinazowahusu maafisa zaidi ya 14 wa shirikisho hilo.Madudu zaidi yanatarajiwa kuibuliwa katika sakata hilo la aina yake katika historia ya mpira wa miguu duniani.
Blatter, 79, sasa amesema kuwa mkutano mkuu wa Fifa unatakiwa kukaa haraka inavyowezekana ili kuitisha uchaguzi mkuu na achaguliwe rais mwingine.Awali mkutano mkuu ulikuwa ukitarajiwa kufanyika Mei 13, mwakani nchini Mexico, lakini sasa inaaminika kuwa mpaka Desemba mwaka huu shirikisho hilo tayari litakuwa na rais mpya.
Hata hivyo, pamoja na kujiuzulu kwake bado kuna kashfa nyingine inachunguzwa jinsi nchi zilivyopewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 ikiaminika kuna rushwa ilitembezwa.

Magazeti ya Leo Jumatano ya Tarehe 3 Juni 2015
Ajinyonga mtini kwa Shati lake.....Kabla ya Kujinyonga Aliwafuata Polisi na Kutaka Awekwe Mahabusu


Mkazi wa Ilembo wilayani Mpanda , Petro Magawe (40) amejinyonga kwa kujitundika mtini akitumia shati lake.

Mtu huyo alijinyonga hadi kufa saa 2 asubuhi juzi karibu na Ofisi ya Misitu iliyopo Mtaa wa Majengo A mjini Mpanda.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari alisema Mei 30 , mwaka huu, Magawe alifika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Mpanda mjini Mpanda, akieleza kuwa alikuwa akihitaji kuwekwa mahabusu .
 
“Badala ya kukubali ombi lake la kuwekwa mahabusu alipata msaada kwa kupewa Fomu ya Polisi namba 3 ( PF 3) ili akatibiwe hospitalini baada ya kuonekana kuwa alikuwa amechanganyikiwa kiakili,” alisema Kamanda.
 
Alisema “Siku iliyofuata asubuhi mtu huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia shati lake mwenyewe.” Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo