Friday, April 15, 2016

Takukuru Yalia na Rushwa Mahakama ya Kisutu


Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ameiomba mahakama iingilie kati kile alichokiita rushwa ya kutisha kwenye taasisi hiyo ya kutoa haki.

Wakili Swai alitoa wito huo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuachia huru mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Geofrey Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe Eva Mhando, katika kesi aliyokuwa akiiendesha. 

Katika kesi hiyo, Mhando, mkewe na maofisa wengine watatu wa zamani wa Tanesco; France Lucas Mchalange, Sophia Athanas Misida na Naftali Luhwano Kisinga, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameibwaga Takukuru baada ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yao.

“Haki haijatendeka na tunatarajia kukata rufaa,” alisema Wakili Swai alipozungumza na waandishi nje ya mahakama.

“Rushwa iliyopo mahakamani inatisha. Serikali inatakiwa kuingilia kati.”

Hata hivyo, wakili huyo hakueleza rushwa hiyo ilifanyikaje katika kesi hiyo ambayo iliendeshwa na taasisi hiyo iliyopewa dhamana ya kuzuia na kupambana na jinai hiyo.

Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Aprili Mosi mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema aliyekuwa akisiliza kesi hiyo, lakini ikaahirishwa hadi Aprili 6, ambayo pia ilisogezwa mbele hadi jana iliposomwa na Hakimu Mkazi Hellen Riwa.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Rusema, Hakimu Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na Tanesco.

Alisema katika mkataba, Mhando, ambaye alikuwa mshtakiwa wa kwanza, alituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutangaza maslahi yake kuwa kampuni ya Santa Clara ni ya Eva Mhando ambaye ni mkewe.

“Suala la msingi la kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo anahusika katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema Hakimu Riwa akisoma hukumu hiyo iliyoandaliwa na Hakimu Rusema.

“Jibu la swali hilo ni kwamba Bodi ya Zabuni ya Tanesco ndiyo iliyohusika na mchakato huo.”

Hakimu Riwa aliongeza kuwa miongoni mwa washtakiwa hao, hakuna hata mmoja aliyekuwa mjumbe katika vikao vilivyoendeshwa na bodi hiyo ya zabuni, wala kuitwa kuhudhuria mkutano wowote wa bodi hiyo.

“Kutokana na sababu hiyo, inawezekana vipi mshtakiwa huyu akatangaza maslahi yake katika mkutano ambao hakuhudhuria?”

Kuhusu suala la mshtakiwa huyo kujua kama Santa Clara inamilikiwa na mkewe na watoto wake, alisema kuwa inawezekana asijue kama wana kampuni.

Alisema kuwa hakuna ushahidi kuwa mshtakiwa huyo aliulizwa swali lolote kuhusu kampuni hiyo.

Katika kusisitiza hoja hiyo, Hakimu Rusema katika hukumu yake hiyo alitoa mfano kuwa mwanamke anaweza kufungua akaunti kwa siri benki na akaweka fedha kisha mumewe asijue.

Kuhusu suala la mshtakiwa wa pili, Eva, kughushi nyaraka na kuziwasilisha Tanesco, alisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa alifanya kosa hilo na kwamba aliyesaini nyaraka hizo ni mtu mwingine ambaye hata hivyo hakushtakiwa.

Wakati wote Hakimu Riwa alipokuwa akisoma hukumu hiyo, baadhi ya watu ambao wanasadikiwa kuwa ndugu wa washtakiwa hao, walionekana wakifanya ishara ambazo zilionyesha wanamuomba Mungu.

Baada ya hukumu hiyo na kuachiwa huru, Mhando alionekana kutoamini na alipotoka mahakamani, alielekea moja kwa moja kwenye gari lake na kukataa kuongea na mtu yeyote.

Hali hiyo ilionekana kuwatia hofu ndugu zake ambao baadhi walimshauri asiendeshe gari, badala yake aendeshwe kwa kuhofia kuwa kwa hali aliyokuwa nayo angeweza kusababisha ajali.

“Msimuachie aendeshe, Mhando kaa kiti cha nyuma,” alisema mmoja wa ndugu zake. Mhando alikubali na kuhamia kiti cha nyuma kisha mkewe naye aliingia kwenye gari hilo na kuondoka viwanja vya mahakama.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 26, 2014 na kusomewa mashtaka na Wakili Swai.



Love to hear what you think!