Friday, April 15, 2016

Anne Kilango Malecela Afunguka Baada ya Rais Magufuli Kumsimamisha Kazi ya Ukuu wa Mkoa wa Shinyanga


Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, ameibukia kanisani na kutoa ya moyoni, ikiwa siku tano baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wake.

Kilango, Jumatatu wiki hii uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.

Hata hivyo, Ikulu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa 45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.

Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa wote, alipokuwa akiwaapisha kuwa wafanya uchunguzi kuhusu uwapo wa watumishi hewa katika mikoa yao na kutoa taarifa.

Kutokana na kutoa taarifa hizo zisizo za kweli, Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wake, akiwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa siku 27. Kilango amekuwa mkuu wa mkoa wa 19 tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.

Mbali na Kilango, Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi, kutokana na taarifa hizo za kutokuwapo watumishi hewa katika mkoa.

Alivyosema Kanisani
Akiwasalimia waumini wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote yaliyomtokea.

“Ndugu waumini wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hata mtu unapojifungua mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.

"Ukiona mzazi wako kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.

Alivyoanza Kazi
Mbele ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), muda mfupi baada ya kuanza kazi, Kilango alisema Shinyanga ni mkoa wenye changamto nyingi ambazo atazishughulikia, lakini atakuwa akilazimika kukimbia Dar es Salaam kumwona mwenzi wake, Mzee John Malecela ambaye ni mgonjwa, na pindi hali yake ikiimarika wataungana naye mjini Shinyanga.

Hayo aliyasema Machi 22, mbele ya wajumbe wa kikao cha kamati hiyo na Ijumaa Machi 25, alisali kanisani hapo.

Sambamba na hayo, aliahidi kupambana na watumishi wazembe na wale wanaoendekeza rushwa na ufisadi na kurejesha hadhi ya mkoa wa Shinyanga kimaendeleo.

Kilango ambaye yuko mjini Shinyanga, akisubiri kukabidhi ofisi kwa mrithi wake kwa mujibu wa utaratibu, bado anaishi hotelini kwa vile aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Ally Rufunga, hajaondoka katika nyumba ya serikali iliyoko Ikulu ndogo, eneo la Lubaga.



Love to hear what you think!