Tuesday, June 2, 2015

Hotuba Ya Mh. Edward Lowassa Aliyoitoa jijini Arusha Wakati Akitangaza Nia Ya Kuomba Kuteuliwa na CCM Kuwa Mgombea Urais Wa Tanzania


UTANGULIZI:

Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,

Hii ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nasema hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia yangu itainakili kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete; wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja kuchukua fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati ya wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.

Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete.
 
 Nikiwa Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80 wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.

Nitaeleza kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa nini naamini mimi ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku muhimu kwangu.

Lakini nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa imara. Na hili pia nitalieleza kwa kina.
Love to hear what you think!