Saturday, December 15, 2012

Mwalimu akutwa mtupu Shuleni Lindi


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Rutamba, Wilaya ya Lindi amekutwa akiwa na nguo za ndani pekee katika usingizi mzito kwenye kibao cha shule hiyo huku akiwa hajitambui kwa madai ya kilichomkutana kinahusishwa na imani za kishirikina.
Tukio hilo limetokea juzi usiku baada ya mkazi mmoja wa kijiji hicho, Juma Mbilemoto kumkuta mwalimu huyo akiwa kwenye kibao hicho wakati alipokuwa anamsindikiza nduguye,Aisha Mbilimoto aliyekuwa anasafiri kuelekea Dar es Salaam.
Akizungumzia tukio hilo, shuhuda huyo alisema alimkuta mwalimu huyo akiwa amelala chini ya kibao cha shule akiwa na nguo ya ndani tu (chupi)huku akikoroma kutokana na kuwa na usingizi mzito.Alisema awali hakumtambua mtu huyo lakini baada ya kumkaribia alimtambua kuwa alikuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo na ndipo alipochukua jukumu la kumwamsha  ili amvalishe kanga, lakini aliikataa na kuondoka kwenda nyumbani kwake akiwa kama alivyokutwa
Kwa upande wao walimu wa shule hiyo walisema kuwa, wamekosa molari wa kufanya kazi kutokana  na kitendo alichofanyiwa mwalimu mwenzao.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Francis Milanzi alisema  walimu shuleni hapo wamekosa amani na kuwasababishia kuzihama nyumba zao  kwa muda na badala yake kwenda kukesha  kwenye ofisi za walimu tangu tukio hilo litokee.
Ofisa elimu wa Wilaya ya Lindi, Cosmas Magigi alisema amepokea taarifa za tukio hilo kwa huzuni na amewaomba walimu kuwa na subira wakati utaratibu wanalishughulikia suala hilo.
Magigi aliongeza kuwa ofisi yake itafanya utaratibu wa kumhamisha  mwalimu huyo na kumtafutia shule nyingine huku akiwataka wakazi wa eneo hilo kujenga ushirikiano na watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Hili ni tukio la pili kutokea katika halmashauri hiyo mwaka huu ambapo la kwanza lilitokea April katika Shule ya Sekondari Ruhokwe, mwalimu wa shule hiyo alilazwa kwenye kibao cha shule  akiwa uchi wa mnyama.



Love to hear what you think!