Saturday, June 22, 2013

MCHUNGAJI AZAA NA HAUSIGELI



Stori:Gladness Mallya na Harun Sanchawa
HAYA ni madai mazito! Mchungaji wa Kanisa la Kiroho la Kijito cha Utakaso au Healing Centre International lililopo Kimara-Mwisho, Dar, Thomas Mariki anadaiwa kuvuliwa kofia ya uchungaji baada ya kutuhumiwa kuzaa na ‘hausigeli’ wake, Sessy Mwambashi.

Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa masikitiko, mke wa ndoa wa Mariki, Joyce Thomas Mariki alidai kuwa yeye na mchungaji huyo walioana mwaka 2004 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Lungai Mwika, Moshi.
Alisema walijaliwa kupata watoto watatu lakini mmoja hakuwa bahati.
MATESO YAANZA
Mwanamke huyo alidai amani katika ndoa yake ilipotea baada ya kujifungua mtoto wa pili (marehemu), mumewe alianza kumtuhumu kuwa alitoka nje ya ndoa na huyo mtoto hakuwa wake.
Aliendelea kudai kuwa, mtoto alipofikisha mwaka mmoja na miezi nane, walishauriana watafute hausigeli ili mama huyo afanye biashara ya kuwaongezea kipato.
Mama mchungaji alisema alimpata Sessy akiwa na miaka 15, mkazi wa Mbozi, Mkoa wa Mbeya.
Alisema yeye alianza biashara ya genge maeneo ya Kimara-Mwisho ambapo alikuwa akiwahi sokoni saa 11:00 alfajiri na kumwacha msichana huyo akiendelea na kazi za nyumbani.

VISA VYAANZA
Mama mchungaji aliendelea kudai: Baada ya miezi michache, mchungaji alibadilika tabia, alikuwa mkali, wakati mwingine alinifuata sokoni na kunipiga akinishutumu nina uhusiano na wanaume ndiyo maana nachelewa kurudi nyumbani.

MUMEWE AMFICHULIA SIRI
Akadai: “Siku moja mchungaji alinifichulia siri kuwa hausigeli wetu ni mjamzito na mimba ilikuwa yake hivyo akataka iwe siri kati yetu watatu.”
Mama Mariki alisema alikubaliana na mumewe ambapo alivumilia kwa kipindi kirefu lakini uzalendo ulimshinda baada ya msichana huyo kuwa na tabia ya kuwatesa watoto huku akisema aachwe kwani ni mjamzito.

MKE NAYE AFICHUA SIRI
Alisema kuwa baada ya kuona mumewe anamjali zaidi hausigeli kuliko yeye na watoto aliamua kwenda kutoa siri kwa wasimamizi wa ndoa, wakaitwa na kusuluhishwa ambapo waliamua kuwa msichana huyo arudishwe nyumbani kwao Mbeya jambo ambalo mtumishi huyo wa Mungu alilitekeleza, yeye mwenyewe alimrudisha msichana huyo kwao.

NDOA YATIBUKA
Mwanamke huyo alidai mumewe huyo aliporudi Dar, alianza visa akisema kuwa hausigeli alikuwa akimpa ‘mambo’ kuliko yeye ambaye amezeeka huku vitisho na vipigo vikiongezeka maradufu!
“Wasimamizi wa ndoa walituita kwa mara nyingine wakatusuluhisha lakini tulipofika nyumbani, mateso yakawa palepale ndipo wasimamizi waliponiambia nirudi kwa wazazi wangu kwani ni aibu kubwa kwa mtumishi wa Mungu kufanya vile,” alisema na kuongeza:
“Kweli nilirudi kwetu Moshi, wazazi wangu walimpigia simu mume wangu kuhusu matatizo yetu, lakini aliwajibu hanitaki na ataniletea talaka nyumbani.”
Alisema miezi mitatu baadaye, wasimamizi wa ndoa walimtaka arudi Dar kwa ajili ya kujua hatima ya ndoa yake.
Aliambatana na kaka yake hadi nyumbani kwa mumewe, cha ajabu walimkuta hausigeli akiwa na mtoto mchanga. Aliwazuia kuingia ndani akidai hawakuwa na mamlaka hayo.
Alisema kaka yake alimtaka hausigeli ampigie simu mchungaji amwambie shemeji yake anamhitaji, alifanya hivyo na mchungaji alifika lakini alipowaona alitoka nduki.

WAZEE WA KANISA WAINGILIA KATI
Aliendelea kudai kuwa ulifika wakati wazee wa kanisa waliingilia kati, wakamuweka mchungaji kikao na kumuuliza kulikoni hawamuoni mke nyumbani badala yake  msichana wa kazi tena akiwa na kichanga.
“Cha kushangaza mchungaji alipandwa na hasira, akawafanyia fujo wazee hao, alimpiga na kiti mzee mmoja ambaye alikuwa msaidizi wake anayeitwa Kisaka na kumjeruhi,” alisema mama mchungaji.
Alisema sakata la kujeruhiwa kwa Kisaka liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Mbezi Kwayusuf na kufunguliwa jalada namba KMR/RB/2125/2013- SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI.

AVULIWA UCHUNGAJI
Alisema katika kikao hicho, wazee hao walifikia uamuzi wa kumvua rasmi uchungaji kwa kumwandikia barua na kumkabidhi.
Mchungaji aliipokea barua hiyo lakini hadi sasa anaendelea na huduma kwani wapo waumini wachache walio upande wake huku wengine wakidaiwa kulikimbia kanisa hilo.

BOFYA HAPA UMSIKIE MCHUNGAJI
Baada ya kuzinyaka habari hizo, Juni 18, mwaka huu, mapaparazi wetu walimtafuta Mchungaji Mariki na kufanikiwa kumkuta nyumbani kwake Kimara-Mwisho ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Siwezi kuzungumzia lolote kuhusu habari alizosema mke wangu kwa sababu suala hili lipo kwenye Baraza la Usuluhishi wa Ndoa na lipo kwa maandishi, naweza kuwaambia kuwa kuna watu wanataka kunipindua, wanapanga hila na njama ili walichukue kanisa na ndiyo wanamtumia mke wangu lakini hawawezi, wameshindwa.
“Kuhusu kuzaa na hausigeli wangu ni kweli na mtoto ana miezi saba sasa, lakini hizo shutuma kwamba alikuwa na miaka 15 siyo kweli, alikuwa na miaka 17 na sasa ana miaka hiyohiyo.”

HAUSIGELI VIPI?
Risasi Jumamosi lilizungumza pia na hausigeli ambaye anaishi na mchungaji huyo kwa sasa kama mke ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Anayesema nilikuwa na miaka 15 ana ushahidi? Wanaoweza kujua umri wangu ni wazazi wangu na ukweli ni kwamba mwezi wa kumi mwaka huu natimiza miaka kumi na nane.
“Kuhusu kwamba nilikuja kufanya nini Dar, nilikuja kwa mume wangu mwenye ushahidi kuwa nilimfukukuza mke wake alipokuja nyumbani aniletee.”
Hata hivyo, Risasi Jumamosi linaendelea kufuatilia sakata hili ili kukujuza nini hatima yake.





Love to hear what you think!