Wednesday, June 17, 2015

MSIMU WA TANO WA AIRTEL RISING STARS WAZINDULIWA LEO

Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo akipiga mpira kuashiria kuzinduliwa kwa michuano hiyo.
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana Tanzania, Ayoub Nyenzi, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano na Rais wa TFF, Jamal Malinzi baada ya kuzinduliwa kwa michuano hiyo.
Wachezaji walioibuliwa kwenye michuano hiyo ambao kwa sasa wapo na kikosi cha timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, kutoka kushoto ni Sherida Boniface, Stumai Abdallah, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Maimuna Hamis, Najihath Abas, Neema Paul na Amina Ally.
Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waliokuwepo kwenye uzinduzi huo.
 MSIMU wa tano wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 inayojulikana kama Airtel Rising Stars, umezinduliwa leo katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel, Kinondoni Morocco jijini Dar.
Michuano ya mwaka huu inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 8 katika mikoa tofauti ikiwa ni hatua ya awali huku ile ya fainali ikifanyika Septemba 11 mpaka 21 jijini Dar ambapo itazishirikisha timu za wanaume za mikoa ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Mbeya, Mwanza na Morogoro na za wanawake ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya na Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema kampuni yao ina nia thabiti ya kusaidia maendeleo ya soka hapa nchini huku wakijivunia mafanikio waliyoyapata kwenye misimu minne iliyopita.
Katika hatua nyingine, Singano alitangaza kampuni hiyo kuingia mkataba na kiungo wa Ivory Coast na Klabu ya Manchester City, Yaya Toure kwenye kampeni yao ya It’s Now yenye lengo la kulea na kukuza vipaji barani Afrika kupitia nyanja mbalimbali za michezo.
Naye mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo, alisema serikali inatambua michuano hiyo kuwa kipaumbele kwenye kuinua soka letu huku Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akiupongeza mpango huo wa kukuza soka la vijana kwani ndiyo msingi wa maendeleo ya soka letuLove to hear what you think!