Friday, October 4, 2013

MTOTO HUYU HAKIKA ANAHITAJI MSAADA WAKO

Stori: Imelda Mtema
HAKIKA ni mateso, tena makubwa. Mtoto Selemani Rajabu mwenye umri wa miaka 17, mkazi wa Ukonga kwa Guta, jijini Dar yuko katika mateso makali baada ya mguu wake mmoja kuvimba mithili ya tairi la gari kiasi kwamba hawezi kufanya jambo lolote zaidi ya kujiburuza tu.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwao akiwa na simanzi kubwa, kijana huyo amesema kwamba anakumbuka amezaliwa akiwa na ulemavu kidogo chini ya nyayo za miguu yake ambazo zilikuwa nene kiasi cha kumfanya ashindwe kutembea na badala yake akawa ni mtu wa kutambaa tu.
Alisema wakati huo alikuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, lakini baadaye wazazi hao walitengana na kumfanya aishi na mama yake huko Pugu Kajiungeni. Kutokana na uwezo duni wa mama yake, alimpeleka hospitali mara moja tu, licha ya mguu wake kuendelea kuvimba kila siku.
“Nakumbuka mama yangu aliwahi kunipeleka hospitali mara moja tu nilipokuwa mdogo, lakini sikumbuki kama aliwahi kunipeleka tena,” alisema Selemani akiwa na sura ya kukata tamaa.
Alisema tangu wakati huo, mguu wake uliendelea kuvimba siku hadi siku mpaka akashindwa hata kutambaa kama mwanzo na sasa akalazimika kujiburuza licha ya uzito mkubwa wa mguu wake kutokana na kuongezeka kwa uvimbe.
Kutokana na hali hiyo kuzidi kuwa mbaya, alisema mwaka jana mama yake alimpeleka Hospitali ya CCBRT ambako baada ya madaktari kumuangalia walisema mguu wake hauna maji ambayo wangeweza kuyanyonya ili kuyatumia kupata vipimo na kujua tatizo linalomsumbua.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mama yake mzazi alifariki na kumlazimu baba yake kwenda kumchukua na kumpeleka kwa bibi yake huko Manzese.
“ Hali ya bibi haikuwa nzuri kiafya, hivyo baba alinichukua tena na kuishi naye kwake nikiwa na mama wa kambo,” alisema Selemani.
Mtoto huyo analalamika kuwa anatamani hata mguu wake huo ukatwe kutokana na adha anayoipata kwani anakosa raha kama watoto wengine wanaotoka nje wenyewe tofauti na yeye anayetolewa kwa kuburuzwa na watu zaidi ya wawili.
“Siku zote na raha kunapokucha najiona kama sina thamani, natamani hata mguu huu ukatwe, siwezi kufanya kitu chochote, natamani kuwa kama watoto wenzangu,” alisema.
Licha ya adha hiyo, Selemani alisema kingine kinachomuumiza ni kufanya haja zote  sehemu alipokaa na hivyo kutoa wito kwa wasamaria, akiwemo Rais Jakaya Kikwete kumsaidia ili aweze kupata matibabu.
Kwa wenye nia ya kumsaidia mtoto Selamani, kwa matibabu au chakula, wanaombwa kuwasiliana na chumba cha habari kwa simu namba 0713 612 533


Love to hear what you think!