Thursday, September 12, 2013

NDOA YA MZEE MAJUTO YAVUNJIKA

Na Imelda Mtema
MWANAMKE anayedaiwa kufunga ndoa ya siri na mchekeshaji mahiri Bongo, Amri Athuman maarufu kama Mzee Majuto au King Majuto, Rahma Abdallah (20), ameibuka na kudai kutelekezwa na mumewe huyo.
Mzee Majuto akiwa na mkewe Rahma Abdallah siku ya ndoa yao.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa kwa siri jijini Dar Julai 28, mwaka huu na kudumu siku 44, inaonekana imevunjika rasmi baada ya Mzee Majuto kutoa talaka kupitia kwa msanii wa filamu aitwaye Rehema Omary.
WOTE NI WAJA LEO, WANDOKA LEO
Akizungumza na gazeti hili katika ofisi zetu, Bamaga-Mwenge, Dar, Septemba 9, mwaka huu, Rahma alidai kuwa alikutana na Mzee Majuto jijini Tanga na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi kwa miezi sita kabla ya kufunga ndoa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliopita.
“Tulifahamiana Tanga, mimi ni mwenyeji wa huko kama ilivyo kwa Mzee Majuto, wakati tukiwa kwenye uhusiano, ulipofika Mwezi wa Ramadhani akaona bora tufunge ndoa ili tusiendelee kutenda dhambi, akaniambia dhamira yake hiyo nami sikukataa,” alisema Rahma.
 
Rahma Abdallah (20).
TOFAUTI MIAKA 40
Mke huyo ambaye ni kibinti cha umri wa miaka 20 aliyepishana na Mzee Majuto kwa umri wa miaka 40 alisema kuwa, mwigizaji huyo alifuata taratibu zote za kufunga ndoa kwa kupeleka barua ya posa nyumbani kwao.
“Alitoa mahari ndipo ilipopangwa siku ya ndoa iliyofungwa nyumbani kwa mama yangu, Mbagala-Zakhem, Dar,” alifafanua Rahma.
ULINZI MKALI, BARAFU MPAMBE
Katika ndoa hiyo iliyofungwa katika Mtaa wa Kibonde-Maji Julai 28, mwaka huu na Shehe Abdurahman Kisoma na kufuatiwa na sherehe nyumbani kwa bibi harusi, ulinzi mkali uliwekwa ili siri ya Mzee Majuto kuoa isivuje.
Mashahidi wa ndoa hiyo walikuwa ni Suleiman Said ‘Barafu’ ambaye ni mwigizaji aliyekuwa mpambe wa bwana harusi pamoja na Mohammed Malila.
...Siku ya ndoa yao.
MAHARI 20,000
Cheti cha ndoa hiyo, kinaonesha kwamba Mzee Majuto alimuoa mwanamke huyo kwa mahari ya shilingi 20,000 aliyolipa yote.
“Baada ya ndoa, Mzee Majuto aliwaomba wazazi wangu nikae nyumbani hadi Mwezi wa Ramadhani utakapoisha ndipo atakapokuja kunichukua, akaniachia shilingi elfu sitini tu, mpaka leo hii sijamuona,” alisikitika mke huyo ambaye alikuwa akijua kama Mzee Majuto alikuwa na mke mwingine.
KAZI KWA PROFESSA J
Mke huyo wa Mzee Majuto alisema kuwa kabla ya kufunga ndoa na gwiji huyo wa uchekeshaji alikuwa akifanya kazi katika saluni ya mwanamuziki Joseph Haule ‘Profesa Jay’ iliyopo Msasani, Dar.
“Nilikuwa nafanya kazi na kupata kipato huku nikiwa nimepanga chumba lakini Majuto aliniambia niache kazi na nirudishe chumba, nami nikafanya hivyo nikijua naenda kuishi kwa mume wangu, kumbe!...” alijuta Rahma.
MESEJI CHAFU ZA MKE MKUBWA
Baada ya Majuto kuondoka mke huyo alikuwa akimpigia simu kutaka fedha za matumizi lakini alikuwa akiambiwa awasiliane na Bi. Rehema, mwanamke ambaye Mzee Majuto huwa anaigiza naye katika filamu zake.
Rahma alilalamika kutumiwa ujumbe wa matusi kwenye simu yake na mke mkubwa wa Mzee Majuto.
“Kitendo hicho kinaniuma sana kwani wakati mwingine huwa ananitukana na kunitishia maisha, akidai eti atanifanyia kitu kibaya, nikimpigia Majuto na kumweleza naye ananijibu mbovu,” aliongeza.
Mke huyo mdogo wa Mzee Majuto alisema kuwa anaumia kutokana na kuharibiwa maisha kwa kuolewa na kuachishwa kazi huku akiendelea kutukanwa na mke mkubwa.
MASHITAKA BAKWATA
Rahma ambaye aliliachia Amani nakala ya cheti cha ndoa alisema msanii huyo amemdhalilisha kwani kila akidai talaka yake anamwambia ameshaituma kwa Bi. Rehema na kumtaka aende akaichukue kitu ambacho ni kinyume na makubaliano yao.
Rahma alisema kuwa amejipanga kwenda kumshitaki Mzee Majuto katika Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ili amlipe fidia na kumtafutia kazi.
“Yeye ndiye aliyenioa lakini nikimdai talaka ananimbia alimpa Bi.Rehema, wakati mwanamke huyo siye aliyenioa, sasa nampeleka Bakwata ili anikabidhi talaka na kunilipa fidia,” alisema kwa hasira mke huyo.
MSIKIE MZEE MAJUTO
Akijibu tuhuma hizo akiwa jijini Tanga, Mzee Majuto alikiri kufunga ndoa na Rahma na kusema kuwa alishamuacha kwa sababu aligundua hajatulia.
“Huyo mwanamke nimeshaachana naye ila kwa sasa anataka kunichafua, kama anahisi ana haki kwa nini asiende mahakamani? Nimemtuma mshenga ampe talaka hataki kuipokea, anataka nije Dar. Kama huo siyo uhuni ni nini? huyo mwanamke hajatulia,” alisema.
TALAKA KULETWA GLOBAL
Mzee Majuto alidai kwamba, Rahma amekuwa akimpa usumbufu na kufikia kumpa masharti ya ajabu na kuahidi kumtuma mtu ailete nakala ya talaka hiyo katika ofisi za (Global).
Love to hear what you think!