Monday, September 30, 2013

UJENZI WA BARABARA ZA JUU (FLYOVERS) KUANZA 2014


MRADI wa Ujenzi wa barabara za juu unaotekelezwa na Serikali ya Japan, unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa 2014. Hayo yalibainika jana baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kufanya majadiliano na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada na kukubaliana kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara za juu na upanuzi wa barabara eneo la Bendera Tatu hadi Kamata. Katika majadiliano hayo, Balozi Okada alimhakikishia Dk. Magufuli kwamba miradi yote inayofadhiliwa na Japan itaanza kutekelezwa rasmi mwanzoni mwa 2014.

Balozi Okada alisema kuwa hivi sasa Japan kupitia kampuni zake za ujenzi, imejipanga kukamilisha miradi yote kwa mujibu wa makubaliano. “Januari 2014 tutaanza na upanuzi wa barabara inayoanzia eneo la Bendera Tatu hadi Kamata, wakati upanuzi huo ukitekelezwa, mchakato wa ujenzi wa barabara za juu unaendelea.

“Kwanza hivi sasa tumeanza mchakato wa kuwapata wakandarasi ambao ni makini kutoka Japan, ambao watatekeleza miradi yote kwa wakati uliopangwa hususani barabara za juu katika eneo la TAZARA na maeneo mengine.

“Hii ni miradi mikubwa sana na inahitaji umakini mkubwa ili kulinda heshima yetu kati ya Tanzania na Japan, katika historia yetu hatujawahi kuharibu kazi kutokana na umakini wetu,” alisema. Kwa upande wake Dk. Magufuli alimhakikishia balozi huyo kwamba taratibu za kusafisha maeneo ya miradi zinaendelea kufanyika na baadhi ya maeneo zimekamilika.

Dk. Magufuli alisema sehemu ya barabara ya kuanzia Bendera Tatu hadi Kamata eneo la Gerezani, limekuwa likisababisha msongamano mkubwa kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba.

Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa ni faraja kubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na watumiaji wanaelekea mikoa ya Kusini mwa Tanzania. Dk. Magufuli alisema mradi wa barabara kuanzia Mwenge hadi Tegeta unaendelea vizuri na kusisitiza mradi huo upo katika hatua za mwisho kukamilika.

“Tunataka kupunguza msongamano wa magari hapa Dar es Salaam, pale Mwenge yamebaki madaraja mawili ambayo yanashughulikiwa, pia zipo sehemu ambazo zilionekana kuwa na kasoro nazo zinarekebishwa. MWISHO

Tarime, Rorya kupata umeme Desemba (pg 2) Na Doroth Chagula, Mara KAZI ya kupeleka umeme katika vijiji 11 wilayani Tarime na Rorya, mkoani Mara, inatarajia kukamilika, Desemba mwaka huu. Kazi hiyo inayotekelezwa na Kampuni ya kizalendo ya Namis Corporate Ltd, inatarajiwa kugharimu, Sh bilioni 7.2.

Mhandisi wa kampuni inayotekeleza mradi huo, Haidu Ruta, alisema utekelezaji wa mradi huo uko katika hatua za mwisho na kubainisha maeneo yatakayonufaika ni pamoja na Hospitali ya Masongo iliyopo wilayani Rorya.

Ruta alivitaja vijiji vya Nyachabakenye, Marasibora na Nyarombo kuwa ni miongoni mwa maeneo yatakayofikiwa, huku wateja 124 wa awali wanatarajiwa kupelekewa huduma ya umeme katika maeneo hayo. Vijiji vingine vitakavyonufaika na mradi huo unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ni pamoja na Kungombe, Kabasa, Salama kati, Mcharo, Sizaki, Chanjunge, Kichumbwa na Shule ya Sekondari Unyari.

Wateja 308 wa awali nao wanatarajiwa kufikiwa na huduma ya umeme, huku wateja 74 katika eneo la Itiryo nao watafikiwa na huduma hiyo. Meneja msaidizi wa ufundi wa REA, Boniface Gissima, alisema awamu ya pili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme inayohusisha wilaya zote za Mkoa wa Mara utagharimu zaidi ya Sh Bilioni 48 na kupeleka umeme katika vijiji 204, huku wateja 14,600, wanatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo ifikapo 2015.


Love to hear what you think!