Monday, September 30, 2013

WATOTO WAFUNGA NDOA! NI TUKIO LA KUSHANGAZA


Wanandoa Mary Chinjendi (15) na Amos Sailowa (17).
Na Imelda Mtema
HAKUNA lugha inayofaa kutumika katika habari hii zaidi ya kusema hii ni kali ya mwaka! Katika hali ya kushangaza, watoto Mary Chinjendi (15) na Amos Sailowa (17), wazaliwa wa Kijiji cha Vilundilo Mbandee, Mkoa wa Dodoma, wamefunga ndoa huku wazazi wa pande zote mbili wakisherehekea harusi, Ijumaa Wikienda lina mkasa wote.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, tukio hilo la kusisimua lilitendeka wiki iliyopita katika kijiji hicho kufuatia Amos kumchumbia Mary na wazazi wa pande zote mbili kuafiki wafunge ndoa huku wasimamizi wao nao wakiwa katika umri wa chini! Dunia ina mambo!
Wanandoa hao wakiwa na wapambe wao siku ya harusi.
BWANA HARUSI AELEZA WALIVYOKUTANA
Baada ya taarifa hizo, Ijumaa Wikienda kupitia kwa mwakilishi wake lilipata mwanya wa kuzungumza na wanandoa hao baada ya kumaliza fungate yao ambapo bwana harusi huyo alikiri kufunga ndoa na Mary au Maria.
Alisema alitokea kumpenda msichana huyo tangu alipomwona kwa mara ya kwanza akipitapita karibu na nyumbani kwao na akavutiwa naye, hasa kwa umbo, sura na mikogo wakati wa kutembea.
“Nilianza kumwona Mary mwaka 2012 akipitapita nje ya nyumba yetu. Kwa kweli alinichengua sana, nikavutiwa kwa uzuri wake wa umbo, sura na mwendo. Hali hiyo ilinichanganya hadi ikabidi nimweleze baba yangu mzazi juu ya upendo wangu kwa Mary,” alisema Amos bila kumung’unya maneno.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
WAANZA UHUSIANO KABLA YA NDOA
Amos alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa baada ya kufikisha ombi hilo kwa baba yake, yeye na Mary wakaanza kuwa marafiki wa ‘baby’, ‘darling’, ‘sweet’ kama siyo laaziz achilia mbali mahabuba.
Anasema wakati huo Mary alikuwa na umri wa miaka 14 tu, lakini kwake hakuona kama ni sababu ya kutompata ili wawe wanapika na kupakua, yeye Amos alikuwa na umri wa miaka 16. Kwa hiyo walikaa mwaka mmoja katika uhusiano. Mh!
Alisema wazazi wa Mary nao walipopelekewa ujumbe wa ushenga wakasema ‘asante Mungu’, wakawa tayari kumpokea Amos kuwa mume wa binti yao mpendwa, Mary.
Maharusi katika pozi.
SIKU YA NDOA YAFIKA
Habari zilieleza kuwa siku ya ndoa hiyo ya kihistoria iliwasili, ndugu, jamaa na marafiki walifika nyumbani kwa mzee Sailowa kwa ajili ya kushuhudia Amos akipata jiko, akipata mke mwema na maandiko matakatifu yanasema mke mwema mtu hupewa na Bwana. Yeleuuwii!
Baada ya ndoa kufungwa, sherehe za harusi ziliendelea nyumbani kwa akina Amos ambapo nyimbo ngoma na nyimbo za asili na kisasa ‘eti mlisema haolewi, mbona kaolewa’ zilitamba na kuifanya harusi hiyo itafsirike kuwa ya kihistoria kwa mwaka 2013 katika kijiji hicho.
WAALIKWA WALA, WANYWA
Licha ya umri wa wanandoa kukosa vigezo vya kuoana, lakini waalikwa waliweza kula, kunywa na kuserebuka huku wakiwatakia maharusi maisha marefu yenye baraka, waje kupata watoto wa kike na kiume na wao waitwe baba na mama.
WASIMAMIZI NI WATOTO WENZAO!
Katika hali ya kuendelea kushangaza zaidi ndoa hiyo ilisimamiwa wa watoto wenzao ambapo ‘matron’ ana miaka 15 na ‘patron’ miaka 16, ambaye naye ameoa huku msimamizi wa kike akisema ana mchumba, Mungu akijalia siku yoyote na yeye atafunga pingu za maisha kama si za milele.
DIWANI AZUNGUMZA
Baada ya tukio hilo, paparazi alimtafuta diwani wa kata hiyo na kumuuliza kama analijua tukio hilo.
“Mimi sikuwepo, nilikuwa kwenye majukumu mengine, lakini suala kama hilo linapotokea huwa linashughulikiwa. Huko nyuma yamewahi kutokea matukio kama hayo, wahusika walifungwa jela.
“Hata hili, kwa sababu ndiyo unaniambia, nitalifuatilia, kama ni kweli wamefunga ndoa wakiwa katika umri wa chini ya miaka ya kisheria ya kumi na nane, watachukuliwa hatua wao na wote walioidhinisha,” alisema diwani huyo.
KAZI YA BWANA HARUSI
Katika mazungumzo yake, Amos alisema kazi inayomfanya apate nguvu ya kuoa kwa mbwembwe ni ufundi seremala ambapo yeye ni stadi katika kazi hiyo.
ANACHOSEMA BI HARUSI
Kwa upande wake bi harusi Mary aliweka bayana kwamba, hana kazi, ila akiwezeshwa anaweza kufanya biashara ya kuuza maandazi.
WAZIRI SOPHIA SIMBA UNALO HILO!
Kwa mujibu wa watu nje ya kijiji hicho ambao walishangazwa na tukio hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba ana kazi kubwa ya kufanya juu ya matukio kama hayo yaliyoshamiri katika jamii.
Love to hear what you think!