Thursday, September 19, 2013

Hakimu achomwa kisu mahakamani


Wauguzi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakimuhudumia hakimu Satto Nyangoha aliyechomwa kisu shavuni jana, akiwa mahakamani na mlalamikaji katika kesi ya wizi wa baiskeli, Emmanuel Izengo. Picha na Suzy Butondo 

Shinyanga. Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake


Love to hear what you think!