Saturday, July 20, 2013

INASIKITISHA SANA AMUUA MKEWE KISA FUTARI


Gladness Mallya na Hamida Hassan
KWELI mapenzi yanaua! Mwanaume mmoja aliyetajwa kwa jina la Dotto, anahusishwa na mauaji ya mkewe, Zainab Bakari, mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Mazishi ya Marehemu Zainabu Bakari katika Makaburi ya Kigogo CCM, Dar.
Tukio hilo la kusikitisha lilijiri hivi karibuni maeneo hayo ambapo Dotto alidaiwa kumchoma mkewe huyo kisu na kusababisha kifo chake baada ya mama watoto wake huyo kukataa kurudiana naye ili ampikie futari katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza na wanahabari wetu, dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Asia Hatibu alisema kabla ya tukio hilo, marehemu Zainab na mumewe Dotto walikuwa mke na mume wa ndoa lakini baadaye walitengana kiaina (bila talaka).
Alisema siku ya tukio hilo, Dotto alimfuata Zainab nyumbani kwa wifi yake alikokuwa akiishi na kumuomba warudiane lakini mwanamke huyo alikataa.
 
Marehemu Zainabu Bakari enzi za uhai wake.
Kitendo cha Dotto ‘kutolewa nje’ na mkewe kilimpandisha hasira na kujikuta akimchoma kisu na kufariki dunia papo hapo.
“Ukweli nimeumia sana kwani muda mfupi alikuwa ametoka nyumbani kwangu ndipo nikaja kuitwa na wifi kuwa nikamuangalie amechomwa kisu na mume wake, baada ya kufika nikakuta tayari ameshafariki dunia,” alisema dada huyo wa marehemu.
Akisimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa, mtoto wa marehemu, Asia Maulid aliyekuwa eneo la tukio alisema alimuona mama yake akiitwa na baba yake na baada ya hapo walianza kuzozana ambapo baba alikuwa akimvuta mama yake huku na kule.
“Nilimuona baba Dotto akimuita mama na alipoenda kuongea naye walianza kuzozana ndipo baba akachukua kisu na kumchoma kwenye sikio.
“Kilichotokea ni kwamba kile kisu kilizama na kutokea sikio la pili, mama akaanguka, damu zikawa zinatoka kwa wingi na baada ya hapo baba alikimbia,” alisema mtoto huyo.
Marehemu Zainabu alizikwa katika Makaburi ya Kigogo CCM, Dar huku mumewe akitokomea ambapo uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini alikokimbilia na sheria ifuate mkondo wake.
Familia ya Zainabu imefungua kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo kwenye Kituo cha Polisi cha Buguruni yenye jalada namba BUG/RB/9165/2013 -MAUAJ
Love to hear what you think!