Saturday, September 21, 2013

DAKTARI FEKI AKAMATWA AKIHUDUMIA WAGONJWA KATIKA HOSPITALI YA MUHIMBILI


DAKTARI anayedaiwa kuwa bandia amekamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, akiwa na vitambulisho bandia vya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) akisomea Shahada ya Pili.
  
‘Daktari’ huyo ambaye amekuwa akitafutwa na uongozi wa chuo kwa zaidi ya mwaka alikamatwa jana asubuhi akiwa hospitalini hapo karibu na jengo kilimo kitengo cha meno.
Katika kitambulisho chake cha kupigia kura anatambulishwa kwa jina la Dismas John Macha aliyezaliwa mwaka 1979 Kilimanjaro na anaishi maeneo ya Upanga Magharibi, Dar es Salaam.

Gazeti hili, lilimshuhudia mtuhumiwa huyo akiwa katika kituo cha usalama cha Muhas na kupekuliwa na askari Polisi wa Muhimbili, Anthony Mwamatepela na kukutwa akiwa na vifaa vya udaktari .

Baadhi ya vifaa alivyokutwa navyo ni pamoja na koti jeupe la udaktari na stetoskopu ambacho ni kifaa cha kusikilizia mapafu yanavyofanya kazi na mapigo ya moyo.

Pia alikuwa na begi jeusi lenye aina mbalimbali za dawa, vitambulisho na karatasi nyingi, lakini alipoulizwa alidai kuwa hizo ni dawa zake.

Macha alikutwa pia na vitambulisho vitatu tofauti, kimoja kikimtambulisha kuwa mwanafunzi wa Muhas wa Shahada ya Pili ya Udaktari (Masters of Medicine ) yenye jina la Macha Dismas kikionesha kusajiliwa kwa namba 60520/2011 na kumaliza muda wake Septemba 30 mwakani. Kitambulisho kingine kilimtambulisha kwa jina la Macha Rogers anayesoma Shahada hiyo hiyo ikionesha kuwa anamaliza masomo yake mwakani.

Alikutwa pia na kitambulisho kinachomwonesha kuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza na kadi ya anuani yenye jina la Amos Nnko ambaye ni Ofisa Rasilimaliwatu wa Chuo hicho.

Akizungumzia alivyomkamata askari wa chuo hicho, Fulgence Semfukwe alisema walimkamata baada ya kupata taarifa za yeye kuwa maeneo hayo na kupanga mbinu za kumkamata.

Alisema saa 4.45 asubuhi jana alimkuta kwenye jengo la meno na kumwomba kwa nafasi yake ya udaktari amsaidie tatizo lake na hivyo waongee pembeni, naye bila wasiwasi akakubali. Alimwuliza anatibu magonjwa gani naye kumjibu anatibu maradhi ya aina nyingi na kumwomba kitambulisho na yeye kumpa cha kwake.

Baada ya hapo alishituka na kudai kuwa ni daktari wa Mwananyamala na amekuja hapo kwa ajili ya kuona wagonjwa wake wa dharura ndipo alipokamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi.

Alisema amekuwa akiwachenga kwa muda mrefu kutokana na kuwa kila walipopewa taarifa yuko wodi au sehemu Fulani hawakumkuta kwani walipishana naye baada ya kuvua koti na kuweka kwenye begi lake jeusi.

Akizungumza na gazeti hili, Macha limweleza mwandishi wa habari hizi kuwa yeye ni mwanafunzi ambaye anaelewa masuala yote ya matibabu, lakini alifeli chuoni hapo mwaka jana.

Alidai kuwa dawa alizokutwa nazo ni zake kwani ana matatizo katika njia ya mkojo na kifua huku akiamua kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.

“Uwezo wa kutibu ninao na nimesoma katika chuo hiki, lakini mwaka jana nilifeli ndiyo maana nikaamua kuwa hivi,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui alisema kutokana na kukamatwa na nyaraka akijitambulisha kuwa mwanafunzi wa ‘Masters of Medicine’, ambaye anaweza kutibu watu hawana uhakika na idadi ya watu ambao ameshatapeli hospitalini hapo.

Kuhusu kusoma Muhimbili, Mtui alikana akisema baada ya kupekua nyaraka za chuo hawakubaini jina la mwanafunzi wa aina hiyo na katika vyeti vyake bandia vinaonesha kusainiwa na Mkuu wa Chuo aliyekuwapo kabla chuo hakijapanda hadhi na kuwa chuo kikuu.

Mtui alisema baada ya kumkamata na kumpiga picha akiwa na mavazi ya udaktari, kumpekua na kumhoji walimpeleka katika kituo cha Polisi cha Selander Bridge kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.

-Habari leo



Love to hear what you think!