Tuesday, April 23, 2013

Tundu Lissu "Matusi Yataisha Bungeni Endapo Spika Ataacha Upendeleo"

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema fujo zitaisha bungeni ikiwa Spika wa Bunge, Naibu na Wenyeviti watafuata na kusimamia kanuni za Bunge bila kupendelea upande wowote.

Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, aliyasema jijini Dar es Salaam jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Alisema fujo hazitaisha kama watu hawatafuata kanuni na Spika kusimamia na kuzingatia mamlaka yake bila ya upendeleo wowote.
“Tatizo kubwa Spika anafanya kazi bila kufuata kanuni za Bunge. Kuna mambo mengine anayatolea maamuzi bila kufuata kanuni za Bunge. Mfano suala letu la adhabu tuliyopewa wabunge watano wa Chadema ya kutohudhuria vikao vitano. Hakuna katika kanuni za Bunge.
Spika alipaswa kupeleka majina yetu katika Kamati ya Maadili ili ichunguze na kupendekeza adhabu kisha ipeleke taarifa bungeni na Bunge ndilo litoe adhabu," alisema.

Alisema kama utaratibu ndani ya Bunge unakiukwa, Chadema wataendelea kupinga hata kama watafukuzwa kila mara kwani wasipofanya hivyo athari yake itakuwa kubwa hapo baadaye.

“Hata kama watu wote watasema niache kuongea, nasema siwezi kuacha mimi ni mbunge na sehemu yangu kubwa ya kazi ni bungeni. Hivyo nikifika huko lazima nitazungumza, kama sitazungumza ndani ya Bunge, nitazungumza nje na nikirudi tena ndani nitalizungumza,” alisema.

Lissu aliongeza kuwa hulka ya Bunge ni kelele na hii si hapa nchini tu, bali hata nchi nyingine, ila tatizo la Watanzania ni uchanga wa mfumo wa vyama vingi na ndiyo maana wanaona mambo hayo kama ni mageni.
CHANZO: ALASIRI


Love to hear what you think!