Sunday, May 26, 2013

Alalamikia anayedai kuleta miradi ya umeme kwa fedha binafsi

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM) ameliambia Bunge kwamba kuna mtu katika Jimbo la Bukoba Vijijini anayejitapa kwa wananchi kwamba miradi ya umeme inayotekelezwa jimboni humo inatokana na fedha zake.
Alisema hatua hiyo inawafanya wananchi kuichukia Serikali kwa kudhani kwamba haitekelezi miradi ya maendeleo bali miradi hiyo inatekelezwa na watu binafsi.
Akichangia kwenye mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni, Rweikiza alisema mtu huyo (bila kumtaja kwa jina) amekuwa akipotosha ukweli wa miradi inayotekelezwa na Serikali ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) akisema anaijenga yeye.
“Mheshimiwa Spika kwa kuwaeleza wananchi kwamba miradi hii inajengwa na mtu binafsi kunawafanya wananchi kudhani kwamba Serikali haiwajibiki kwao, nafurahi sasa Waziri kupitia hotuba yake ameeleza ukweli kwamba miradi hii ya umeme inatekelezwa na Serikali na si mtu binafsi na wananchi wajue kwamba mtu huyu ni mwongo anawadanganya wananchi,” alisema.
Katika kusambaza umeme vijijini na hivyo Serikali inawajibika kuongeza fedha zinazotengwa ili kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini ili kuchochea maendeleo katika maeneo hayo hatua itakayosaidia pia kukuza Pato la Taifa.
Alisema pamoja na jitihada hizo za kusambaza umeme katika vijiji vya Bukoba Vijijini lakini bado yapo maeneo ambayo umeme unapita juu lakini chini wananchi wakosa umeme hatua ambayo inaathiri maendeleo kwa wananchi wa vijiji hivyo na hivyo ni lazima REA isambaze umeme katika vijiji hivyo haraka.
Akizungumza nje ya Bunge, Rweikiza alimtaja mtu huyo anayepotosha wananchi kuwa miradi ya umeme ya Serikali ni yake amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo na amewahi pia kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne (Nazir Karamagi ) akidai anataka kujipatia umaarufu wa kisiasa.


Love to hear what you think!