John John Mnyika awasilisha ushahidi wizi BoT !!!

Hatimaye
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewasilisha ushahidi wa
awali kwa Katibu wa Bunge, kuhusu tuhuma alizozitoa bungeni
dhidi ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, kwamba ni
mmoja wa watuhumiwa katika kashfa ya ukwapuaji wa mabilioni ya fedha
uliofanywa katika Akaunti ya Malipo ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Hatua
hiyo imechukuliwa na Mnyika kutekeleza maelekezo aliyopewa na
Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama, ambaye alimpa siku saba
kuwasilisha ushahidi kuthibitisha kauli yake hiyo.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mnyika katika kikao cha Mkutano wa Bunge unaoendelea
hivi sasa mjini hapa, kilichofanyika, Julai 3, mwaka huu, katika
mjadala kuhusu makadirio ya mapato ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma. Siku hizo ziliisha juzi.
Kwa mujibu wa Mnyika, ushahidi huo aliuwasilisha kwa Katibu wa Bunge, mjini hapa juzi.
“Kuhusu
tuhuma dhidi ya Mwigulu Nchemba, ushahidi wa awali nilishawasilisha
leo (juzi) ndani ya siku saba kama ilivyotakiwa,” alisema Mnyika.
Katika
mkutano huo uliotawaliwa na mvutano, malumbano, hisia kali na maneno
ya kashfa miongoni mwa wabunge, Mnyika pamoja na mambo mengine, alisema
Nchemba aliwahi kuwa mtumishi wa BoT, ambayo ilikumbwa na kashfa hiyo
na kwamba, naye ni mmoja wa watuhumiwa.
Kauli hiyo ya Mnyika ilimfanya Mhagama kusimama na kumpa Mnyika siku hizo awe amewasilisha ushahidi wa kauli yake.
Kwa
upande wake, Nchemba wakati akichangia mjadala wa Bunge, alisema
alijiunga na BoT mwaka 2006 wakati huo ukwapuaji wa fedha BoT
ulikwishafanyika.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alithibitisha kuwasilishwa kwa barua ya maelezo ya Mnyika.
“Ni kweli tumepokea jana barua ya maelezo lakini Spika atawaelezeni kesho (leo),” alisema.