MASIKINI KAPUYA, TAMWA, TGNP NA LHRC WAMWANDAMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa,Valerie Msoka Chama cha Wanahabari
Wanawake Tanzania (Tamwa), kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP) na Kituo cha Msaada wa Kisheria (LHRC), kimelaani
viongozi wanaotumia madaraka yao, nafasi zao na nguvu zao kisiasa
kuwadhalilisha watoto wa kike.
Mashirika hayo yanayotetea haki za wanawake na watoto, yamesema
yamesikitishwa na habari zilizozoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya
habari kuhusu wasichana wawili wanaotafuta haki yao dhidi ya kiongozi wa
kiserikali anayetuhumiwa kuwadhalilisha.
“Mashirika hayo yanafahamu kuwa vitisho vilivyotolewa na kiongozi
huyo vimewasababishia wasichana hao kuogopa kuishi nyumbani kwao kwa
kuhofia maisha yao,” ilisema sehamu ya taarifa ya pamoja ya mashirika
hayo.
Iliongeza: “Tunashangazwa kuona hakuna hatua zozote zilizochukuliwa
na mamlaka husika wakati wasichana hao wakitafuta msaada,” alisema
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, katika taarifa hiyo.
Masharika hayo yametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuwalinda wasichana hao dhidi ya mtuhumiwa.
Aidha, ili kujenga imani na utawala bora, mashirika hayo yamemtaka mbunge huyo kujiuzulu mara moja.
Alisema Tamwa, TGNP na LHRC, yanawataka Watanzania kuungana na kupinga
viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya. Watanzania wapige vita vitendo
visivyo vya haki kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheri.