MWANANCHI
Hamasa ya wanaCCM kutangaza nia ya
kuwania urais imemwibua mwanafunzi Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma
katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Maliki Malupu.
Malupu alitangaza nia ya kugombea urais
kupitia CCM akiahidi kushughulikia suala la elimu, afya, kilimo na
michezo huku akijua kuwa umri wake haujatimia miaka 40 inayotakiwa
kikatiba.
Akitangaza nia hiyo mjini Morogoro jana,
Malupu alisema kutokana na uaminifu na uadilifu wake, ameamua kuwania
nafasi hiyo pamoja na mambo mengine kwa kuwa ni haki yake kikatiba.
Alipoulizwa atatimizaje nia yake hiyo
bila kuwa na sifa kikatiba, alisema vifungu vya katiba vinavyotaja umri
vina utata, hivyo ameamua kuingia kuvitafutia suluhisho.
“Unajua
ibara ya 39 (1) (b) inasema lazima utimize miaka 40, lakini ibara (d)
inasema mtu mwenye sifa za kuwa mbunge au mjumbe wa baraza la
wawakilishi anaweza kuwania urais,” alisema akifafanua kuwa yeye ana sifa hizo.
Akieleza sababu nyingine zilizomsukuma
kuwania urais, Malupu alisema kuwa ni kuhakikisha sekta ya elimu
inaboreshwa kikamilifu kwa kuwa muda mrefu imekuwa ikichezewa na baadhi
ya viongozi.
Alisema muundo wa sekta hiyo unapaswa
kurekebishwa kwa ama kufutwa au kuondoshwa utaratibu wa kupanga viwango
vya ufaulu wa GPA kwa wanafunzi wa elimu ya sekondari katika mitihani ya
kidato cha sita na cha nne.
Alisema utaratibu huo haufai kwa kuwa
hautoi matokeo ya kuboresha maarifa kwa wanafunzi, pia unawaathiri
wanafunzi kisaikolojia katika kujitofautisha wao na wanafunzi wa elimu
ya juu.
“Nitahakikisha
naboresha mitalaa kwa masomo ya kidato cha nne na cha sita ili kuleta
weledi wa kina na wa kutosha, nitaboresha mazingira ya watumishi sekta
ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na stahiki za walimu wa
msingi hadi vyuo,” alisema.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),
mwaka huu, unaingia kwenye uchaguzi ukiwa na safari ya uhakika na siyo
ya matumaini kama ilivyotolewa na mmoja wa watangaza nia ya kugombea
urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Dk Slaa alisema, kauli hiyo ni moja kati
ya nyingi zinazotolewa na viongozi wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambazo Watanzania wamechoka kuzisikia na badala yake wanahitaji vitendo.
Alitoa kauli hiyo juzi mjini Tunduma
wilayani Momba mkoani Mbeya, alipokuwa akihutubia wakazi wa mji huyo
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.
Dk Slaa alisema Watanzania wanahitaji
safari yenye uhakika wa maendeleo ambayo watayapata Oktoba, mwaka huu,
kupitia upinzani lakini siyo kutoka kwa kiongozi yeyote wa CCM.
“Eti
safari ya matumaini, hivi kweli Tanzania iliyojaa kila aina ya madini na
utajiri wa kutisha halafu tunasema safari ya matumaini badala ya
vitendo? Watanzania tumechoka na kauli za matumaini, tumechoka kuishi
kwa matumaini katika nchi yetu,” Dk Slaa.
Mbali na hilo, Dk Slaa aliwashangaa
baadhi ya watangaza nia wa CCM walioiponda Serikali yao kwamba
imeshindwa wakati wao ndio walitakiwa kuwa mstari wa mbele kuondoa kero
hizo.
Akizungumza kuhusu Ukawa walivyojipanga
kuingia Ikulu Oktoba mwaka huu, Dk Slaa alisema wana akiba ya kutosha ya
viongozi makini wa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Alisema wakishika dola hawatakuwa na sababu yoyote ya kukopa viongozi kutoka kwa CCM.
“Hatuna
njaa ya viongozi ndani ya upinzani, tunao wa kutosha. Hatuna haja ya
kwenda CCM kuwakopa viongozi, Oktoba tupeni ridhaa upinzani tubadili
sura ya nchi,”.
MWANANCHI
Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara Yanga wametumia milioni 300 kwa usajili wa wachezaji saba mpaka sasa.
Tayari Yanga imewasajili wachezaji wanne wapya Denis Kaseke kwa milioni 35 kutoka Mbeya City, Malimi Busungu milioni 25 kutoka Mgambo JKT, kipa Benedicto Tinocco kwa milioni 5 kutoka Kagera Sugar pamoja na Haji Mwinyi wa KMKM kwa milioni 25.
Pia imewaongezea mikataba Haruna Niyonzima kwa miaka miwili kwa gharama ya milioni 140, Mbuyu Twite mkataba wa mwaka mmoja kwa milioni 50 pamoja na Deogratius Munishi ‘Dida’ kwa milioni 20.
Yanga imeshafunga usajili wake kwa
wachezaji wa ndani na sasa imebakiza nafasi kwa wachezaji wa kimataifa
na inasubiri kwanza majibu kutoka kwa Shirikisho la soka TFF ianze
usajili mara moja.
Yanga na Azam zimetuma maombi TFF
kuitaka kuongeza idadi ya wachezaji wa kimataifa kutoka watano na sasa
kufikia 10 ili kuimarisha vikosi vyao hasa katika michezo ya kimataifa
MTANZANIA
Mbio za kusaka urais kwa makada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo
kwa mara ya kwanza katika historia ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani
Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio hizo.
Akitangaza nia yake katika eneo la
Mwitongo kijijini Butiama jana, Makongoro aliwashambulia makada wenzake
ndani ya CCM ambao wanaongoza makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni
‘vibaka’ wanaokivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada
wanaoongoza makundi ndani ya chama hicho, Makongoro aliwataja kwa majina
kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu
wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuendesha makundi ya urais na akahoji
sababu za kutafuta cheo hicho cha juu kwa fedha.
CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho, alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa
kweli na anataka kuirudisha nchi katika misingi ya uadilifu endapo CCM
itampa ridhaa ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba
mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani
ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni kibaka
tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele atabaki
kuwa kibaka tu.
“Wananijua
vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo wanaotuvurugia
chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,” Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa
mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa
ndani ya CCM na alisema baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha
makundi na mipasuko isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia
kuwapo makundi ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo
imechochea badhi ya viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wakiwamo
wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi
kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya
viongozi hao kuishi maisha ya kusukumwa kwa upepo wa makundi
yanayomilikiwa na watoa fedha.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona
watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu aliyeiomba kazi
hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai kukukuongoza maana
hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili ajinufaishe,” Makongoro.
MTANZANIA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametegua kitendawili kuhusu hatima ya madai ya wananchi katika mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Lukuvi amesema kutokana na hali hiyo
kuanzia sasa kila mwananchi mwenye kiwanja au nyumba yake atalazimika
kuuza kiwanja chake kwa bei anayoitaka au kujenga nyumba kwa mujibu wa
ramani ya mji mpya
Akizungumza na wananchi hao juzi katika
mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere Kigamboni Dar es Salaam, Lukuvi, alisema sintofahamu iliyokuwapo
ilitokana na hapo awali wananchi kutowekwa wazi kuhusu mchakato wa
uuzaji wa maeneo yao.
“Wananchi
wamekuwa katika sintofahamu juu ya uuzaji wa maeneo yao, wengine
mnafikiri Serikali ndiyo itakayonunua ardhi yenu na wengine mnafikiri
ardhi inadalaliwa na Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji Mpya wa
Kigamboni (KDA),” alisema Lukuvi na kuongeza;
“Hakuna
Serikali itakayouza ardhi wala KDA kudalalia ardhi yenu…wananchi wa
Kigamboni ndiyo mtakaoamua juu ya uuzaji wa ardhi yenu na serikali
itakuwa mwangalizi ili wananchi wasiibiwe kwa kuuza bei ya chini sana,”
Alisema wananchi wanachotakiwa ni
kuchagua mambo matatu katika mpango huo ambayo ni kuuza ardhi yao
wenyewe moja kwa moja kwa wawekezaji, kuingia ubia na wawekezaji na
kutafuta fedha za kujenga wenyewe.
Alisema kama mwananchi ataamua kujenga mwenyewe atatakiwa kufuata ramani na mpango wa mji mpya unavyoonyesha.
“Mtu
anaweza kuamua kujenga mwenyewe lakini si kwamba unaamua kujenga
unachotaka bali utajenga kilichopo kwenye mpango, haiwezekani eneo la
kujenga majengo makubwa ya biashara wewe ujenge choo,”Lukuvi.
Alisema ili kuhakikisha wananchi
wanatekeleza mambo hayo matatu ni lazima wapatiwe hatimiliki za maeneo
yao suala ambalo awali halikuwapo kwa madai kuwa hakuna haja ya kutoa
hati kwa eneo ambalo tayari lipo kwenye mpango.
MTANZANIA
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni imesema
Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiba sera yake ya
elimu inayozungumzia elimu bure kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.
Mbali na hilo, wapinzani wameonya makada
wa chama hicho wanaotangaza nia ya kuwania urais kuacha kutumia sera
hiyo ya upinzani kwa sababu walikuwa Serikalini tangu uhuru na
wameshindwa kufanya hivyo.
Msemaji Mkuu kwa kambi hiyo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo,
alisema elimu haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za CCM kwa awamu
zote za utawala wake na ndiyo maana imeshindwa kutekeleza hata Ilani
yake ya uchaguzi.
“Sera
ambayo CCM imepigia upatu kwa miaka yote 53 ya uhuru na ambayo pia
imeshindwa kutekeleza ni kilimo, ndiyo maana tangu enzi za uongozi wa
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere sera zilizosikika ni Siasa ni
Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa na
sasa Kilimo Kwanza. Hatujawahi kusikia elimu kwanza kwa utawala wa CCM
kwa miaka yote 53 ya Uhuru,” alisema.
Suzan ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu
(CHADEMA) alisema sera ya elimu kwanza ni ya upinzani na kwamba ipo
katika ilani ya uchaguzi ya Chadema ya mwaka 2005 na 2010 na imepewa
kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu.
“Itakumbukwa
kwamba Chadema iliposema elimu bure kama ingechaguliwa kuunda serikali
mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda chafu ya kuwapotosha
wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure.
“Lakini
ili kuthibitisha ile methali isamayo kwamba njia ya muongo ni fupi, CCM
hivi sasa imekubali kula matapishi yake na kusema katika kipengele cha
3.1.5 cha sera mpya ya elimu ya mwaka 2014 kwamba elimu itakuwa bure,” :
Kuhusu sera mpya ya elimu, alisema
imekuwa hazitekelezeki kwa kuwa ni sera bainishi na imekuwa ikibainisha
upungufu pekee na kuacha sehemu ya utekezaji.
“Tanzania
imekuwa ikisifika kwa kuandika vizuri sera zake, lakini utekelezaji
wake ni shida. Mfano sera hii haielezi ni kwa kiasi gani itaondoa
ubaguzi au matabaka ya elimu hasa viwango vya elimu. Pia haielezi nini
maana ya kufuta ada ikiwa kuna michango mingi kuliko ada yenyewe,” alisema.
Awali akiwasilisha hotuba yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imetekelezwa.
Alisema sekta ya elimu imefanikiwa kwa
asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya
kwanza ya mikakati hiyo.
NIPASHE
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema amemshukia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdularhman Kinana,
kwamba anamchonganisha na wapiga kura wake kwa kudai kuwa serikali
imetoa Sh. milioni 400 katika jimbo hilo kupitia Mfuko wa Jimbo wakati
siyo kweli.
Mrema alisema ni jambo la kushangaza kwa
Kinana kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kumchonganisha na wapiga
kura wake, ili CCM ijijengee mazingira mazuri katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu.
“CCM
kwanini mnaanza kushiriki uongo, mnataka kunichonganisha kwa wapiga kura
wangu ili kuning’oa Vunjo, nawahakikishia CCM hang’oki mtu Vunjo, hizo
Sh. milioni 400 hazijaletwa jimboni kwangu labda mmepeleka kwa wabunge
wa CCM,” .
Mrema alisema mbinu zinazofanywa na CCM kumshambulia katika jimbo lake kama mpira wa kona haziwezi kuzaa matunda.
HABARILEO
Sekta ya Elimu imefanikiwa kwa asilimia
81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Matokeo ya utekelezaji wa mikakati
iliyowekwa na BRN ni kupanda kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya
Msingi (Darasa la Saba) na kupanda ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu
ya Sekondari (Kidato cha Nne).
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa aliyasema hayo bungeni jana wakati alipowasilisha
Bajeti ya Mwaka 2015/16.
Dk Kawambwa alisema, “Kwa mujibu wa
taarifa ya mwaka mmoja (2013/14) sekta ya elimu imefanikiwa kwa asilimia
81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya
mikakati hiyo.”
Aliyajata baadhi ya mafanikio ambayo
yamehakikiwa na ‘Presidential Delivery Bureau’ ni kutoa tuzo kwa shule
na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba na
kidato cha nne.
Alisema jumla ya tuzo 3,044 zilitolewa
kwa shule zilizopata ufaulu uliotukuka na zile zilizopanda kwa ufaulu
ikilinganishwa na mwaka 2013.
Pia alisema walimu 4,103 wa masomo ya
Sayansi, Hisabati na Lugha walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa
kutambua wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kumudu masomo.
Aidha, alisema ujenzi wa miundombinu ya
shule 47 za sekondari kati ya 264 zilizolengwa katika awamu ya kwanza
ulikamilika. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule 1,200
katika awamu tatu.
“Madeni ya shilingi 1,852,162,158.21 ya malimbikizo ya mishahara yalilipwa kwa watumishi 916 wa wizara,” aliongeza Dk Kawambwa.
Alisema matokeo ya utekelezaji wa
mikakati hiyo ni kupanda kwa ufaulu wa darasa la saba kutoka asilimia
50.6 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 56.99 mwaka 2014.
“Na kupanda kwa ufaulu wa Mtihani wa
kumaliza Elimu ya Sekondari (Kidato cha Nne) kutoka asilimia 57.09 mwaka
2013 hadi kufikia asilimia 69.76 mwaka 2014,” alieleza Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi.
Akizungumzia utungaji wa Sera za Elimu,
alisema rasimu ya andiko la uanzishwaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu
imekamilika, na kuwasilishwa katika mamlaka husika.
Aidha, alisema katika mwaka 2014/15,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitoa mikopo kwa wanafunzi
99,590 wakiwemo 2,117 wa Stashahada ya Elimu ya Ualimu wa masomo ya
Sayansi na Hisabati.