Thursday, September 26, 2013

POLISI WAMZOA BWANA NA BI HARUSI WAKATI WAKIFUNGA NDOA NA DIFENDA

Binti wa miaka 14, Zubeda akiwa tayari kufunga ndoa na Hamis (35).
Stori: Gladness Mallya
NDOA iliyokuwa tayari kufungwa na shehe kati ya Hamis Ngaumba (35), mkazi wa Bangulo, Ulongoni, Gongo la Mboto, Dar na binti wa miaka 14 anayetajwa kwa jina moja la Zubeda, imesambaratishwa na polisi wa Kituo cha Polisi cha Sitaki-Shari, Dar kutokana na umri wa bi harusi kuwa mdogo, Amani limeidaka hiyo.
Hamis Ngaumba (35) aliyetaka kumuoa binti wa miaka 14.
Kizaazaa hicho cha aina yake kilichovuta hisia za wengi kilitokea saa 10:00 jioni, Jumapili iliyopita ambapo Shehe Bakari Mgesa wa Msikiti wa Bangulo alikuwa ameanza kutoa mawaidha ya maandalizi ya kufungisha ndoa hiyo lakini ghafla polisi na mapaparazi waliingia na shughuli kuishia hapo.
ISHU ILIKUWA HIVI
Mapema siku ya tukio, msamaria mwema ambaye hakupendezwa na kitendo hicho alitoa taarifa kwa mapaparazi ambao nao waliwataarifu polisi wa Kituo cha Polisi Sitaki-Shari na kupewa maafande kutoka dawati linaloshughulikia unyanyasaji wa kijinsia na kuambatana nao hadi eneo la tukio.
BREKI YA KWANZA KWA MJUMBE
Kabla ya kufika eneo la tukio, breki ya kwanza ilikuwa ni kwa mjumbe wa eneo hilo Shina Namba 10, Erasto Nyakiege ambaye alikiri kusikia taarifa hizo za mtoto kufungishwa ndoa lakini alizipata muda mfupi kabla polisi na waandishi hao kufika eneo hilo.
MJUMBE AUNGANA NA POLISI, MAPAPARAZI
Mapaparazi, polisi na mjumbe huyo waliambatana hadi kwenye nyumba ambayo ilikuwa na shamrashamra za ndoa hiyo na kumkuta shehe akijiandaa kufungisha huku waalikwa wakiwa wameshakaa mkao wa kula ‘mnuso’ (pilau).
MSHTUKO WATOKEA, WATU WAKIMBIA
Mshtuko mkubwa ulitokea eneo la sherehe baada ya watu kuwaona askari, wengine walikimbia kama wanafukuzwa na simba. Bi harusi yeye alikimbilia chumbani huku bwana harusi akijichanganya katikati ya wageni waalikwa lakini polisi walimweka ‘mtukati’.
SHEHE AWA WA KWANZA KUSIMULIA
Akizungumza baada ya kunaswa, Shehe Bakari alisema ndiyo kwanza alikuwa anajiandaa kwa zoezi la kuwafungisha ndoa wawili hao lakini kama angebaini kuwa mtoto huyo ana miaka isiyokidhi vigezo, asingekubali kwa vile hata dini ya Kiislamu hairuhusu mtoto kuolewa mpaka atimize miaka 18 na kuendelea.
BI HARUSI AWA WA PILI KUWEKA BAYANA
Naye bi harusi, Zubeda ambaye anaishi na bibi yake aitwaye Bibi Abuu, alieleza kuwa ndoa hiyo ilikuwa ni kama utani kwani mwanamme huyo alikuwa akimtania tangu akiwa mdogo akimwambia kuwa akikua atamuoa, hivyo akawa anamuita mchumba lakini hakuwahi hata siku moja kumtongoza.
MAHARI ILIVYOPELEKWA
Zubeda alisema cha kushangaza siku moja aliwaona wazazi wa kijana huyo wakipeleka barua ya posa na mahari na kumkabidhi mjomba na bibi yake kwani baba yake mzazi anaishi Shinyanga na mama anaishi Tabora, tangu akiwa mdogo anaishi na bibi yake huyo.
“Mimi natamani sana kusoma lakini sina uwezo kwani niliishia darasa la tatu baada ya wazazi wangu kushindwa kunisomesha ndipo bibi akaja kunichukua ndiyo maana suala la kuolewa limenitokea tu bila mwenyewe kupenda. Ilikuwa kama utani lakini wakapokea mahari,” alisema Zubeda huku akilia kwa uchungu.
BIBI AZUNGUMZA HUKU AKIWA AMELEWA TILALILA
Bibi Abuu alipoona mambo yameharibika huku akiwa  tilalila alikimbilia ndani kulala ambapo babu wa kufikia wa Zubeda, James alisema ni kweli mjukuu huyo ana miaka 14 na kuongeza kwamba waliopokea mahari ya mtoto huyo kiasi cha shilingi laki tano na nusu (550,000) ni wajomba pamoja na Bibi Abuu lakini yeye hajui chochote kuhusiana na ndoa hiyo.
KIUMENI WADAI MAHARI
Baada ya sekeseke hilo, ndugu wa upande wa mwanamme walikuja juu na kudai mahari yao huku wakitishia kwamba kama hawatarudishiwa basi wakwe hao watapelekwa polisi kwani hata wao hawakujua kama huyo anayeolewa ni mtoto wa miaka 14.
WAPELEKWA POLISI
Hata hivyo, polisi waliwazoa ndani ya difenda bwana harusi, bi harusi na wajomba wawili ambao ndiyo waliopokea mahari na kwenda kuwaweka nyuma ya nondo kusubiri taratibu za kisheria.




Love to hear what you think!