Saturday, January 3, 2015

PANYA ROAD WALIVYOTIA HOFU WAKAZI DAR

 
Polisi wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova.
Jana usiku Jiji la Dar es Salaam wakazi wake walijawa na  taharuki, hofu na wasiwasi mkubwa kwa saa mbili baada ya kundi maarufu la waporaji lililojulikana kama  Panya Road, kudaiwa kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali.
Taarifa zilizoenezwa na watu wasiojulikana zilidai kuwa  kundi hilo lilikuwa linapora watu katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo zilienea kwa kasi ya ajabu kupitia mitandao ya kijamii  na ujumbe mfupi wa simu.

Wananchi wakikimbia usiku wa jana jijini Dar es Salaam.
Baada ya maeneo ambako kundi hilo lilidaiwa kufanya uporaji ni Tabata, Magomeni Kagera, Sinza, Mwananyamala, Kinondoni, Kijitonyama, Manzese, Kigogo na Buguruni, huku wanafunzi wanaoishi katika Hosteli za Chuo Kikuu Dar es Salaam, wakitoka nje ya mabweni yao kwa kuhofia kuvamiwa na kikundi hicho.
Taharuki hiyo iliyoanza saa mbili usiku, ilisababisha wakazi wa maeneo mengi ya jiji kujifungia ndani, huku wafanyabiashara wakifunga maduka na kujificha wakihofia kundi hilo la wahalifu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura alipotafutwa kuzungumzia hilo alikana kutokea kwa tukio hilo. “Hakuna kitu kinachoitwa Panya Road, huo ni uvumi tu wananchi walikuwa wanavumisha,” alisema.
Wakati Kamanda Wambura akikanusha, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu aliwaambia waandishi wa habari kuwa makamishna wa polisi walikuwa wanakutana hiyo jana kwa dharura kwa ajili ya kulichukulia hatua jambo hilo.
Alisema katika kikao hicho alimuagiza kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova kufuatilia na kwenda kwenye vyombo vya habari kulizungumzia.
Kamanda Kova naye alijitokeza kwenye runinga usiku huo na alikanusha kuwepo kwa Panya Road na akasema naye atakesha kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.




Love to hear what you think!