Monday, September 30, 2013

KIKWETE"WANAO MWAGIA WATU TINDIKALI TUTAWAKOMESHA"


RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali yake imedhamiria na itahakikisha inalimaliza tatizo la watu kumwagiwa tindikali, iwe ni Visiwani Zanzibar au Tanzania Bara. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Rais Kikwete amesema hivi karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni katika mitaa ya Zanzibar na kukamata watu 10 wanaodaiwa kushiriki katika mipango ya kuandaa na kutekeleza matukio ya watu kumwagiwa tindikali.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam, ilisema Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi jijini New York Marekani, alipokuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, baada ya kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa kutaka ufafanuzi wa suala hilo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, chanzo cha tatizo la watu kumwagiwa tindikali lina sura nyingi, lakini kutokana na jinsi Serikali ilivyojipanga, tatizo litafikia mwisho baada ya siku chache.

“Ni kweli tumekuwa na vitendo hivyo, zaidi Visiwani Zanzibar kuliko Tanzania Bara ambako nako pia vimekuwapo vitendo hivyo.

“Ni jambo la kulaaniwa sana na hivi karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni maalumu na msako mkubwa Tanzania Visiwani ambako watu 10 walitiwa mbaroni na watafikishwa katika vyombo vya sheria baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

“Wakati tatizo hili lilipoanza, tulidhani kuwa alikuwa ni Sheikh Soraga aliyekuwa anatafutwa peke yake na watu ambao walikuwa hawakubaliani kisiasa na msimamo wake, lakini mara wakaanza kushambuliwa watu wengine wakiwemo wasichana wawili wa Uingereza ambao walikuwa wanafanya kazi za kujitolea tu, lakini, tatizo hili ni lazima likome,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali wakati baadhi ya wananchi wameshadhurika kwa tindikali.

Miongoni mwao ni kiongozi maarufu wa Kiislamu Visiwani Zanzibar, Sheikh Soraga ambaye alimwagiwa tindikali wakati akifanya mazoezi ya viungo katika mitaa ya mji wa Unguja.

Mbali na huyo, viongozi wengine wa kidini wa Kanisa Katoliki visiwani humo, wameshamwagiwa kemikali hiyo na pia wasichana wawili raia wa Uingereza waliokuwa wakifanya kazi za kujitolea Visiwani Zanzibar, nao walimwagiwa kemikali hiyo.

Wasichana hao baada ya tukio hilo lililotokea mwezi uliopita, walisafirishwa kutoka Zanzibar na kuletwa Dar es Salaam kisha wakasafirishwa kwenda nyumbani kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.


Love to hear what you think!