Monday, September 16, 2013

Kesi ya WAZIRI MKUU PINDA yaanza kusikilizwa...Serikali yatoa pingamizi kali


Kesi inayomkabili waziri mkuu Mizengo  Pinda na mwanasheria mkuu wa serikali  imetajwa mahakamnai kwa mara ya  kwanza ambapo  wamewasilisha pingamizi  la  awali dhidi ya  kesi ya kikatiba waliyofunguliwa na kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu  kwa kushirikiana na chama cha wanasheria Tanganyika.
  
Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS,wanadai kuwa Pinda alivunja katiba kutokana na kauli  aliyoitoa bungeni hivi karibuni  wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi  wakati wa vurugu. 
 

Hata hivyo Pinda na  mwanasheria mkuu  kwa pamoja katika majibu yao ya madai hayo, wamewasilisha pingamizi la awali ambapo  pamoja na mambo mengine wamedai   kuwa walalamikaji na watu  walioorosheshwa katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo.
 

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la  majaji watatu likiongozwa na jaji kiongozi, Fakihi Jundu akisaidiana na jaji Dk Fauz Twaib na jaji Augustine Mwarija ambapo  upande wa wadaiwa uliwakilishwa na mawakili wa serikali wakuu watatu, Nickson Mtingwa, Sarah Mlipana na Alesia Mbuya.
 

Aidha  upande wa walalamikaji uliwakilishwa na mawakili wanne kati ya saba waliotajwa  awali .Akizungumza na waandishi  wa habari nje ya mahakama hiyo,  mmoja ya mawakili hao amesema  wamepewa siku  14 kujibu pingamizi lililotolewa .
 

Wakati kesi hiyo ilipotajwa mahamani hapo  upande wa madai uliomba siku 21 kuwasilisha  majibu ya wadaiwa ambapo hata hivyo wakili wa serikali mkuu, Mtingwa, alipinga ombi hilo katika kipengele cha muda ulioombwa na badala yake  akapendekeza wapewe siku 14 tu.
 

Mahakama katika uamuzi wake uliosomwa na jaji kiongozi Jundu, ilikataa ombi la wadai na kukubaliana na ombi la wadaiwa, na kuwapa wadai siku 14 badala ya siku 21 kama walalamikaji walivyomba ili kuweza kuwasilisha majibu yao.
 

Mahakama hiyo iliamuru wadai wawasilishe mahakamani majibu yao  kabla au septemba 30, na kupanga kusikiliza pingamizi la awali la wadaiwa oktoba 18.
 
Itakumbukwa kuwa pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, katika mkutano wa 11 wa bunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu bungeni, juni 20,2013.Love to hear what you think!