Sunday, May 26, 2013

MWANAMKE MCHAWI ADONDOKA KANISANI AKIWA UCHI WA MNYAMA JIJINI DAR


Wakati Mtwara kukilipuka kwa vurugu za gesi na kusababisha maafa, jijini Dar kumeibuka taharuki ya aina yake baada ya mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Anna kudaiwa kuwa ni mchawi na kudondokea kanisani.

Tukio hilo lililochukua saa kadhaa lilitokea katika Kanisa la Yesu Kristo la Huduma ya Maombezi na Uponyaji linaloongozwa na Nabii Flora Peter lililopo Mbezi Beach Salasala, Dar hivi karibuni.
 
Taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo ambao ni waumini wa kanisa hilo inadai kuwa mwanamke huyo, mkazi wa Bunju, Dar alifika kanisani hapo saa 4:45 asubuhi huku akiwa amebeba Biblia na pochi lake akionekana kuwa sawa waumini wengine.

Ilidaiwa kuwa muda mfupi baada ya maombi kuanza, katika hali isiyo ya kawaida, mwanamke huyo aliruka kupitia dirishani akapotea na kuacha waumini vinywa wazi.

 
Habari zilidai kuwa kuna baadhi ya watu walimuona kwenye paa ya nyumba ya watu waliojenga karibu na kanisa hilo, hali iliyozidi kusababisha mkusanyiko mkubwa wa watu wakiwemo askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliokuwa wakimshangaa.
 
Wakati taharuki hiyo ikiendelea, mwanahabari wetu alitonywa kuwepo kwa tukio hilo ambapo aliwasha ‘tukutuku’ yake na kuwahi eneo la tukio.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa viongozi wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Octavian Mahembe alikuwa na haya ya kusema: 
 
“Nakumbuka kulikuwa na waumini wengi kanisani, walikuja kwa ajili ya maombi, huyo mwanamke naye alikuja hapa kama waumini.

“Ilipofika saa 5:00: asubuhi watu wakawa wanasubiri maombi, baadaye nabii naye akawa amefika na kuanza kutoa maombi. Baada ya maombi kuanza, yule mwanamke alianza kuhangaika, akawa anahamahama, hatulii sehemu moja.

“Watu waliokuwa wanataka kuombewa waliambiwa wapite mbele.


“Yule mwanamke alikurupuka na kurukia ukuta wa futi sita na nusu, akadondoka nje.

“Nabii alisema afuatwe ili aombewe, alidai kwa kuwa si mtu mwema ni hatari na anaweza kuliangamiza kanisa na waumini kwa jumla kwani alikuwa na nguvu za giza.

“Alipochukuliwa akapelekwa kwa Nabii, akaombewa sala ya toba huku akikataa kwa kusema hana dhambi.
 

“Aliendelea kuombewa na baada ya maombi alitoka nje kupitia mlangoni. Akiwa nje alivua nguo na kubaki na ile ya ndani tu, akapanda juu ya paa la nyumba jirani na kanisa, akarukia nyumba nyingine juu kwa juu bila kushuka.
 

“Hakuishia hapo, akawa amerukia mti huku akionekana kama mtu wa ajabu kiasi kwamba hata watu wengine hawawezi kufanya yale aliyokuwa akiyafanya.

“Watu wengi walikusanyika wakiwemo polisi na wanajeshi. Baada ya kupotelea mitini, ghafla kilisikika kishindo kanisani baada kudondoka eneo hilo.

“Baadaye alipelekwa ofisi ya serikali ya mtaa kwa usalama wake kwani watu walitaka kuchukua sheria mikononi wakidai ni mchawi,” alimaliza kusimulia kiongozi huyo wa kanisa.

Hata hivyo, habari nyingine zilidai kwamba kabla ya mwanamke huyo kupelekwa serikali ya mtaa, wakati akiombewa alikuwa akitangaza mambo mengi aliyokuwa akiyafanya yasiyoeleweka kwa watu wasiojua mambo ya kilozi.

Mwandishi wetu hakuishia hapo, alikwenda hadi ofisi za serikali za mtaa kutaka kujua kama mwanamke huyo alifikiswa hapo na sehemu alipo kwa sasa.
 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Salasala, Monica Timba alikiri kutokea kwa tukio hilo akidai kuwa siku hiyo hakuwepo ofisini lakini alipigiwa simu na mkazi wa eneo lake kujulishwa juu ya tukio hilo.
 

“Niliambiwa kuna vurugu kubwa katika mtaa wangu na kwamba kulikuwa na mchawi amedondoka kanisani,” alisema mwenyekiti huyo.
 

Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa  baada ya kupewa taarifa hiyo alimpigia simu mtendaji wake, Ramadhan Juma ili mwanamke huyo aokolewe na walifanya hivyo.

Alisema kuwa baadaye mwanamke huyo alipelekwa kituo kidogo cha polisi kilichopo eneo hilo cha Mtongani. 



Love to hear what you think!