Saturday, May 18, 2013

KESI YA ‘RAMA MLA WATU’ YAZUA TIMBWILI MAHAKAMANI

Stori:Richard Bukosi, Dar
MAMA wa marehemu Salome Yohana, Pendo Dustan Mushi (picha ndogo katikati) ambaye kichwa cha mwanaye huyo kinadaiwa kukutwa na Ramadhan Suleiman ‘Rama mla watu’ amezua timbwili Mahakama Kuu, jijini Dar akitaka kujua hatma ya kesi hiyo ya mauaji.
Tukio hilo lilitokea Mei 16, mwaka huu ambapo mama huyo alinaswa na kamera yetu akilalamika huku akilia kwa uchungu akitaka kujua hatma ya kesi hiyo ya mwanaye ambayo imedumu tangu mwaka 2008.
“Nataka kujua hatma ya kesi ya mauaji ya mwanangu, mara kwa mara nimekuwa nikija hapa mahakamani na kurudi bila kujua chochote kinachoendelea.
“Inaniuma sana kuona hukumu haitolewi, licha ya mwanangu kupoteza uhai muda mrefu lakini siwezi kumsahau, nimekuwa nikilia kila nikikumbuka kifo chake na hasa siku za kesi ndiyo huwa naumia sana,” alilalamika mama huyo na kuongeza:
“Hata mwenendo mzima wa kesi siufahamu, nilisikia kwenye vyombo vya habari kuwa kesi yake inasomwa leo lakini mpaka dakika hii sielewi chochote.”
Baada ya kulalamika sana, mama huyo alipata msaada wa kufikishwa kwa makarani wa kesi za jinai mahakamani hapo ambao walimhakikishia kuwa kuwa kesi hiyo itatajwa Mei 24, mwaka huu mbele ya Jaji John Temba wa mahakama hiyo.
Rama ambaye alijizolea umaarufu mkubwa mwaka 2008 baada ya kukamatwa akiwa na kichwa cha mtu kinachodaiwa kuwa ni cha Salome, hadi sasa anasota Gereza la Segerea Jijini Dar akisubiri mwenendo wa kesi hiyo.


Love to hear what you think!