Saturday, May 11, 2013

ASKARI ALIYEMUUA MTOTO MDOGO WA RISASI AKAMATWA......CHADEMA WAANDAMANA, POLISI YAJIBU MAPIGO


ASKARI Polisi wa Kituo cha Tarime mkoani Mara mwenye namba D. 4662 Koplo Mathew, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za uzembe uliosababisha kifo kwa risasi cha mwanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya Msingi Rebu, Deus Jacob (9).

Kifo hicho kilitokea wakati polisi wakiwa kwenye harakati za kukamata mtuhumiwa, Marwa Bisara, mkazi wa kitongoji cha Songambele kata ya Sabasaba mjini hapa, aliyekuwa akituhumiwa kwa shambulio na kudhuru mwili.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni katika kitongoji cha Songambele, baada ya Koplo Mathew na askari wenzake wakiwa na mlalamikaji, wakifuatilia mtuhumiwa na kumkuta na wenzake katika pagala wakivuta bangi.
 
Wakati polisi wakijiandaa kumkamata, mtuhumiwa Bisara alimvamia Koplo Mathew akitaka kumnyang'anya bunduki na katika purukushani hiyo, risasi zilifyatuka na moja kumpata Deus kichwani na kumuua papo hapo baada ya kichwa kufumuka.

Kamanda Kamugisha alisema chanzo cha mauaji ni mtuhumiwa Bisara kukaidi amri ya kukamatwa. Lakini mwenzake Julius Maseke (38) mkazi wa mtaa wa Ronsoti alikamatwa akiwa na misokoto 47 na kilo 3.25 za bangi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
 
Polisi ilitoa mwito kwa raia wema kutoa taarifa kwa vyombo husika watakapomwona Bisara na inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele alionya wanasiasa waache kulitumia tukio hilo kisiasa kwa kuwa marehemu Deus hakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. 

Alionya hivyo kwa alichokisema ni baadhi ya wafuasi wa Chadema kuchocheana kufanya vurugu wakihamasishana kuchukua mwili wa marehemu huyo na kufanya maandamano kwenda Bomani ziliko ofisi za Mkuu wa Wilaya na Kituo cha Polisi.


 Hata hivyo, maandamano hayo yalizimwa na Polisi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na mwili huo uko katika mochari ya hospitali ya wilaya na unatarajiwa kuzikwa leo.Love to hear what you think!