. Hatuwezi, Hatuwezi!... Mchakamchaka, Chinja, Mchaka mchaka, chinja!
Ndugu zangu,
Utotoni
niliwasikia kaka na dada zangu wakiimba wimbo huu wa mchakamchaka
uliojaa hisia za utaifa. Ni kwenye mchakamchaka wa shuleni kila
asubuhi.
Naam, hata wakati huo kulikuwa na utata wa masuala ya mpaka kati ya Tanzania na Malawi . Zilikuwa ni enzi za Rais Kamuzu Banda.
Na
Watanzania hatukuwa na ukame wa nyimbo za kebehi dhidi ya Banda.
Mwingine uliimbwa hivi; " Kipara cha Banda kina ukoko!" Hakyamungu.
Hata wakati huo kulikuwa na harufu ya vita baina ya ndugu wawili;
WaMalawi na WaTanzania. Maana, ukweli sisi ni ndugu wa damu.
Kuna
hata simulizi za kweli za Watanzania upande wa pili wa Ziwa Nyasa
waliokesha kusheherekea Uhuru wa Malawi. Hivyo basi, tunaweza kabisa
kidiplomasia kutamka, kuwa "Jambo la Malawi ni letu!" Ndio, shida yao ni
yetu, furaha yao ni yetu.
Na
tushukuru kuwa JK wetu ni mwanadiplomasia. Nitakuwa mtu wa mwisho
kuamini kuwa JK anaweza kutuingiza katika ' Vita vya kiwendawazimu'
dhidi ya jirani na ndugu zetu wa Malawi.
Na
picha hiyo hapo juu inaongea; JK na JB ( Joyce Banda), wanazungumza
kwa furaha kama ndugu. Wawili hao hawatoi nafasi kwa wachonganishi wale
wa enzi za ugomvi wa utotoni. Maana, utotoni ilikuwa hivi, kaka zetu
walipotaka kufurahia wadogo zao tukipigana makonde, walisubiri pale
mmoja anapomkasirikia mwenzake. Haraka atatokea kaka na mchanga mkononi.
Atatamka kwa mmoja kati ya wawili walio mbele yake;
"
Haya, puta mchanga wangu kama kweli wewe ni mwanamme!" Nani asiyetaka
kuwa mwananme? Atauputa mchanga. Kisha kaka anamgeukia mwingine; " Haya
sasa, nilipie ng'ombe wangu!".
Kulipa ng'ombe ilikuwa na maana ya kuanza kurusha konde. Na hapo ugomvi ulianza rasmi!
Na
kuna miongoni mwetu wenye kutamani vita. Anayetamani vita ni mtu
mjinga. Mwalimu alipata kutamka; " Vita si lelemama". Na katika dunia
hii inasemwa; Chagua vita vyako. Vita vingine havina lazima ya
kupiganwa.
Na
tofauti zetu na Malawi zinaweza kutatuliwa kwa mazungumzo ya kindugu
kama anavyoonekana JK pichani akiongea na dada yake; JB- Joyce Banda.
Na
wala hatuwahitaji tena akina Moses Nnauye kututungia nyimbo za
Mchakamchaka. Eti twende tukiimba; " Banda ( Joyce) Wa Malawi, Katuvalia
Kitenge Cha Ngozi Ya Mamba, Kututishia Watanzania, Hatuwezi,
Hatuwezi!".
Naama. Wakati umebadilika.
Maggid Mjengwa,
Iringa.0788 111 765
http://mjengwablog.com