Msemaji
wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah
Mwambene akitoa ufanunuzi kwa waandishi wa habari jana mjini Dar es
salaam juu ya taarifa zilizochapishwa na gazeti la Malawi News kuwa
Wamalawi waishio nchini Tanzania wanaogopa kutoka nje kutokana na
ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania taarifa ambazo sio kweli.
Msemaji
wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah
Mwambene akiwaonyesha waandishi wa habari jana mjini Dar es salaam
kichwa cha habari cha gazeti la “Malawi News” kinachosemeka “MALAWIANS
FACE XENOPHOBIA IN TZ” ambacho kilichapishwa na gazeti hilo kuhusu madai
ya kubaguliwa raia hao wa kutoka Malawi jambo ambalo sio kweli.
Na Benedict Liwenga-MAELEZO_Dar es salaam
SERIKALI
ya Tanzania imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la nchini
Malawi lijulikanalo kama “Malawi News” kuwa Wamalawi waishio nchini
Tanzania wamekuwa wakiogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa
na Watanzania.
Kwa
mujibu wa Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya
Habari Assah Mwambene amesema kuwa taarifa hizo ni za kupotosha umma na
kuleta chuki dhidi ya Tanzania na nchi jirani na hazina ukweli wowote
ule.
Bw. Mwambene ameongeza kuwa hakuna raia yeyote wa kutoka Malawi aliyebakwa wala kunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine.
“Hakuna
mwananchi yoyote kutoka Malawi aliyebakwa , wala hakuna raia yoyote wa
Malawi aliyepo hapa nchini anayeogopa kutoka nje kwa sababu ya ubaguzi
wowote ” amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Amesema
kuwa licha Tanzania kuwakamata wahamiaji haramu 1030 kutoka Malawi,
Serikali ya Tanzania iliwapa fomu ili kama walikuwa wanahitaji kuishi
nchini wahalalishe uwepo wao hapa Tanzania kwa wale wote walionyesha nia
ya kuendelea kuwepo hapa nchini .
Aidha wahamiaji wote haramu 1030 kutoka Malawi waliachiwa huru na wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhalalisha uwepo nchini.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa mpaka sasa kati wahamiaji haramu 1030 hakuna
aliyewekwa ndani ama kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kosa la kuwepo
kinyume.
Kufuatia
taarifa hizo ,Mkurugenzi huyo amelitaka gazeti hilo kusahihisha taarifa
hiyo na kuiomba radhi Tanzania kwa upotoshaji huo na kuongeza kuwa
kauli hiyo ni sawa na matusi kwa Tanzania.
Aidha
amesema kuwa hadi hivi sasa zaidi ya wahamiaji haramu 24,000 kutoka
Jamhuri ya Kidemokarisia ya Kongo (DRC) , Rwanda, Burundi , Uganda na
Zambia wamerejeshwa makwao kwa kosa la kuishi Tanzania bila vibali.