Jana Club ya soka ya Azam
ilitangaza kwamba Mchezaji wao Mrisho Ngasa tayari amepelekwa Simba kwa
mkopo ambapo Simba walipewa sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngasa
mshahara wake kamili (TZsh 2,000,000) kwa mwezi pamoja na stahiki zake
nyingine zote za kimkataba.
Sababu za kumpeleka Ngasa kwa
mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam FC ingetoa kwa Ngasa
kama angebaki Azam Fc, Pia iliwekwa wazi kwamba Azam haijamlazimisha
Ngasa kwenda Simba kama inavyopotoshwa, Kama Ngasa anataka kuvunja
mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na dola 50,000 na
Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo simba
lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC.
Azam ilisema “Tunaomba kuweka
msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngasa na kuvunja mkataba wake na
hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngasa hataki kwenda tunakompeleka
Azam FC inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu, Lakini Ngasa na
washauri wake waelewe kuwa akiamua kubaki Azam FC atakaa nje ya uwanja
kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba wake, kwani Azam FC haipotayari
kumvisha jezi mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu”
Azam ilisema kosa alilolifanya
Ngasa ni kubusu na kuvaa jezi ya Yanga wakati bado ni mchezaji wa Azam
hivyo ilionekana ni kitendo cha nidhamu mbovu na kuidhalilisha brand ya
Azam.