Richard Bukos na Haruni Sanchawa
Mkazi wa Bunda mkoani Mara, Elisha Makumbati anadaiwa kumfanyia ukatili wa kupindukia mkewe, Nasra Mohammed (38) (picha ndogo juu) kwa kumburuza na gari uvunguni, umbali wa mita 150 baada ya kutokea kutoelewana kufuatia wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na gazeti hili dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mwanne Daudi, ambaye alishuhudia tukio hilo alisema:
“Mdogo wangu alifanyiwa ukatili wa kutisha na mumewe kwani Februari 2, mwaka huu mimi na Nasra tulikuwa tunatoka kwenye saluni moja iliyopo mtaa wa Posta, maeneo ya Bunda.
“Tukiwa njiani ghafla tulimuona Elisha ambaye ni mumewe akiwa kwenye gari aina ya Nissan Patrol lenye namba za usajili T 400 BBC na kulisimamisha mbele yetu kisha akamuita mdogo wangu kwa…
Richard Bukos na Haruni Sanchawa
Mkazi wa Bunda mkoani Mara, Elisha Makumbati anadaiwa kumfanyia ukatili wa kupindukia mkewe, Nasra Mohammed (38) (picha ndogo juu) kwa kumburuza na gari uvunguni, umbali wa mita 150 baada ya kutokea kutoelewana kufuatia wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na gazeti hili dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mwanne Daudi, ambaye alishuhudia tukio hilo alisema:
“Mdogo wangu alifanyiwa ukatili wa kutisha na mumewe kwani Februari 2, mwaka huu mimi na Nasra tulikuwa tunatoka kwenye saluni moja iliyopo mtaa wa Posta, maeneo ya Bunda.
“Tukiwa njiani ghafla tulimuona Elisha ambaye ni mumewe akiwa kwenye gari aina ya Nissan Patrol lenye namba za usajili T 400 BBC na kulisimamisha mbele yetu kisha akamuita mdogo wangu kwa hasira.
“Nasra alivyoenda akamuuliza mumewe, kwa nini alitaka kuwagonga, wakaanza kulumbana na kushutumiana kwa wivu wa kimapenzi,” alisema Mwanne.
Dada huyo wa marehemu aliendelea kusema huku akitokwa na machozi: “Baada ya kumaliza malumbano yao mimi na Nasra tulianza kuondoka, ghafla tukashtukia mumewe akiondoa gari kwa kasi na kumgonga mkewe na kumburuza kwa umbali wa mita 150 kwa mujibu wa kipimo cha jeshi la polisi lililopima ajali hiyo.
“Wakati akimburuza mdogo wangu mimi na umati uliokuwa ukishuhudia tulipiga mayowe ya kumtaka Elisha asimamishe gari lakini aliendelea kuongeza mwendo huku damu zikitapakaa barabarani mpaka alipokwenda kukutana na tuta ndipo mwili ukachomoka uvunguni mwa gari.
“Mdogo wangu Nasra wakati akisagika kwenye lami mimi nilikuwa nikilikimbiza gari hilo kwa nyuma. Nilipofika eneo alilochomoka nilimkuta askari wa usalama barabarani ameshafika na tayari alianza kupima ajali hiyo na muda si mrefu lilifika gari la polisi ‘Difenda’ na kumpakia Nasra na kumpeleka Hospitali ya Bunda, maarufu kama DDH.
“Alipopimwa aligundulika amevunjika mbavu saba zilizosababisha kutoboa mapafu, mguu wa kushoto na kupata majeraha makubwa mgongoni na sikio la kushoto lilikuwa limenyofoka, kutokana na hali hiyo alihamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza na kufikishiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Dada huyo wa marehemu alizidi kusema: “Hali ya mdogo wangu iliendelea kuwa mbaya ambapo Juni 16, mwaka huu, Hospitali ya Bugando ilimpa uhamisho wa kwenda Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambapo alifikishiwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU)
“Akiwa Muhimbili madaktari walimtoa nyama za sehemu mbalimbali na kumrudishia mgongoni baada ya kuona nyama yote ya mgongoni zilitoka na kujikusanya sehemu ya makalioni.
“Marehemu mdogo wangu aliendelea kuugulia maumivu ambapo Jumanne iliyopita, saa saba za usiku aliaga dunia na tumemzika kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar,” alisema Mwanne huku akifuta machozi na akadai mtuhumiwa mpaka sasa yupo huru mitaani.
Juhudi za gazeti hili kuzungumza na mtuhumiwa huyo ziligonga mwamba baada ya simu zake za mkononi kutopatikana hewani.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya amelaani kitendo hicho na kulitaka jeshi la polisi nchini kumkamata mtuhumiwa huyo.