Siku moja baada kifo cha
mwandishi wa habari Daudi Mwangosi wa Channel 10 kutokea kwa kulipukiwa
na bomu Iringa akiwa mikononi mwa polisi waliokua wakiwatawanya wafuasi
wa Chadema, waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu Tanzania
wametoa kauli.
Jukwaa la wahariri Tanzania
limesema limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwandishi
huyo ambae alikua mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Iringa.
Jukwaa limesema tukio hilo
linaiingiza Tanzania kwenye historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji
wa uhuru wa habari kwani ni kwa mara ya kwanza inashuhudiwa mwandishi
akiuwawa kazini.
Nacho chama cha waandishi wa
habari Dodoma kimelaani mauaji hayo na kusema hakina tena imani na jeshi
la polisi na kinahitaji tume itakayoundwa kuchunguza kifo hicho
ishirikishe wanahabari, asasi za kiraia na mashirika yasiyokua ya
kiserikali ili haki itendeke.
Kwenye line nyingine ni kwamba
kituo cha sheria na haki za binadamu Tanzania kimesema kinajiandaa
kulishitaki jeshi la Polisi katika Mahakama ya uhalifu wa kimataifa The
Hague Uholanzi kutokana na kuendelea kusababisha mauaji kwa raia wasio
na hatia mara kwa mara.