Sunday, April 21, 2013

Wabunge wa Chadema kuweka kambi majimbo ya Makinda, Ndugai

Wabunge sita wa Chadema waliosimamishwa bungeni wameamua kwenda kuwashtaki Spika Anne Makinda na Naibu wake Job Ndugai kwenye majimbo yao.
Wakitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Mbugani, Mwanza jana, walisema pia watakwenda kwenye majimbo ya wabunge wawili wa CCM, Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera) ili kueleza jinsi wabunge wa upinzani wanavyokandamizwa bungeni.

Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Kongwa (CCM), aliwasimamisha wabunge sita wa Chadema kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kutokana na kile alichokiita kufanya vurugu bungeni. Hatua hiyo ya Ndugai aliyoichukua Aprili 17, mwaka huu ilipata baraka za Spika Makinda Ijumaa iliyopita.

Wabunge waliosimamishwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ezekiah Wenje (Nyamagana). Katika mkutano huo ulioanza saa 9.30 alasiri na kumalizika saa 12.00 jioni, ulihudhuriwa na wabunge wanne kati ya hao. Mbilinyi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhutubia akifuatiwa Mchungaji Msigwa, Kiwia na Wenje. Lissu na Lema hawakuhudhuria.

Akizungumzia ziara yao katika majimbo ya viongozi hao wa Bunge, Mchungaji Msigwa alisema itakuwa ya kuwashtaki kwa kuendesha Bunge kuwapendelea wabunge wa CCM hata wanapofanya makosa ya wazi.

Alidai kuwa wabunge wa CCM ndiyo vinara wa lugha chafu bungeni na kuwatolea mfano Mwigulu na Lusinde. Pia alizungumzia tusi zito lililotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, Aprili 17, mwaka huu.
“Kila mtu alimshuhudia Serukamba alipoporomosha tusi zito, lakini Spika na Naibu wake hawakuchukua hatua zozote.

“Lissu na sisi wengine tumeadhibiwa kwa kosa la kuomba mwongozo wa Spika. Hapa wananchi mnaona kuna haki kweli,?” alihoji Mchungaji Msigwa huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Alisema watapita kwenye majimbo ya wabunge wa chama hicho waliosimamishwa ili kuwaelimisha wapigakura wao.

Alisema wataanza ziara majimboni kesho wakianzia Iramba Magharibi kumshtaki Nchemba. Baada ya hapo watakwenda Singida Mashariki kwa Lissu ili kuwapa ukweli wapigakura wake.
Mchungaji Msigwa alisema baada ya hapo watakwenda Kongwa kwa Ndugai na kisha Mtera kwa Lusinde kabla ya kuelekea Njombe Kusini kwa Makinda. Pia watakwenda Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha.

Hata hivyo, ziara ya wabunge hao kwenda mkoani Mbeya imekwaa kisiki baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athumani Diwani kukataa kutoa kibali.

Kumlipua kigogo CCM
Mchungaji Msigwa ameahidi pia kulipua bomu la kigogo wa ngazi ya juu wa CCM, ambaye alidai kuwa anajihusisha na ujangili wa meno ya tembo atakaporejea bungeni baada ya kumaliza adhabu yake wiki hii.

Wenje ataja safu ya 2015
Wenje aliwaambia wafuasi wa chama chake kuwa kimejipanga kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2015 na CCM wanapaswa kujipanga kuondoka madarakani.

Alitoa kali alimpotaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa kuwa Rais na Freeman Mbowe, Waziri Mkuu. Wengine aliowataja na kuwapa vyeo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Waziri wa Fedha), Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Kilimo), Lema (Mambo ya Ndani), John Mnyika (Nishati) na Wenje (Mambo ya Nje).


Love to hear what you think!