SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka (pichani), kurejea nchini akitokea Afrika Kusini kwa matibabu, sasa hajulikani alipo.
Taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia zinasema kuwa familia hiyo imekuwa ikihofia maisha ya ndugu yao mara tu baada ya kutua nchini kutoka Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa kutokana na kutekwa na kuumizwa vibaya na hatimaye kutelekezwa katika Msitu wa Mabwepande na watu wasiojulikana, hivyo sasa wamemtorosha nyumbani kwake na kumpeleka wanakojua wao.
“Alikotoroshewa ni siri ya ndugu na jamaa zake, hawataki kabisa watu wajue,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kutoroshwa kwa Dk Ulimboka kunatokana na hofu waliyokuwa nayo wanafamilia kwa madai kuwa maadui wa ndugu yao wanajua kile walichomfanyia na wanatambua kuwa maadam sasa ana akili timamu, anaweza kuwataja.
Waandishi walifunga safari hadi Ubungo Kibangu ambako inahisiwa anaweza kupatikana Dk. Ulimboka lakini matokeo yake waandishi wetu walipofika na kuuliza wenyeji wa nyumba iliyotajwa walijibiwa kuwa hayupo na walipotaka kujua yupo wapi, watu hao walisema hawajui.
“Siyo rahisi kumuona Dk Ulimboka ndugu zangu, kila mtu hana imani na mtu anayetaka kuongea na daktari hata baadhi ya ndugu nafasi hiyo hawaipati,” alisema mtu huyo ambaye hakutaka kujitambulisha jina.
Habari zaidi zilidai kuwa baada ya kurejea nchini, Dk Ulimboka alitua kwa Mchungaji Josephat Gwajima kwa ajili ya kuombewa na kumshukuru Mungu kwa madai kuwa alinusurika kifo.
Taarifa zinadai kuwa baada ya kutoka kanisani hapo alienda Bagamoyo ambapo chanzo hicho hakijui alifika huko kwa lengo gani. Waandishi wetu walikwenda kanisani lakini hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kumzungumzia Dk Ulimboka kwa madai kuwa msemaji ni Gwajima mwenyewe.
BABA MZAZI
Wiki iliyopita baba mzazi wa Dk Ulimboka alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hayuko tayari kuongea lolote kuhusu mwanaye na kwamba yote amemwachia Mungu.