SIKU chache zimekatika baada ya tukio la kusambaa mitandaoni kwa picha tata zenye pozi kati ya mheshimiwa Komba na mrembo aliyejulikana kwa jina moja la Angel.
Hatimaye mrembo huyo ameibuka na kuanika mambo mazito kama si makubwa, Risasi Mchanganyiko linakudadavulia.
Awali katika gazeti hili toleo la Jumamosi iliyopita ukurasa wa mbele
kulikuwa na habari hiyo ikiwa na kichwa; KHAA! KOMBA! Katika habari hiyo
picha zilizomuonesha mheshimiwa Komba akiwa na mrembo huyo zilipamba
ukurasa huku mwenyewe (Komba) akidai ni picha za kutengeneza).
OFM YAINGIA MITAANI
Kwa vile Komba alikataa picha si zake huku baadhi ya vyombo vya dola
kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) vikitangaza
kuingia kazini kumtafuta sosi wa picha hizo, ilibidi timu makini ya
Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ kutoka Global Publishers iingie kazini
kumsaka mrembo huyo kwa udi na uvumba.
YATUMIA NUSU SIKU
OFM ambayo huwa haishindwi kitu, ilitumia nusu siku ya Ijumaa iliyopita
na kufanikiwa kuinasa namba ya simu ya mkononi ya Angel pamoja na picha
nyingine ikiwepo iliyotumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili.
Aidha, ilibainika kwamba, mrembo huyo anaitwa Angel Kissanga, mkazi wa
Kinondoni jijini Dar es Salaam, bila ajizi Paparazi wetu alimwendea
hewani Angel na kumuuliza kama ana habari zozote kumhusu yeye.
Angel: “Habari kama zipi? Mimi sina habari zozote.”
Paparazi: “Hujaona kwenye mitandao ya kijamaii wameweka picha zako ukiwa katika mapozi tata na mheshimiwa Komba?”
Angel: “Ngoja kwanza, nitakupigia.”
MUDA UNAKWENDA, ANGEL ARUDIWA
Baada ya kuona muda unakatika bila mrembo huyo kupiga simu kama
alivyokuwa ameahidi, paparazi wetu alimrudia hewani ambapo safari hii
simu yake ilipokelewa na mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni dada wa
Angel.
“Mimi si Angel, ni dada yake. Angel amepandwa na presha baada ya wewe
kumwambia kuna picha zake na mheshimiwa Komba kwenye mitandao.
“Unajua ngoja nikuambie ukweli. Mdogo wangu ameshtuka sana, hivi hapa tupo Hospitali ya Micco Sinza, amelazwa.”
PAPARAZI ATIA TIMU HOSPITALINI
Kusikia hivyo, paparazi wetu alifunga safari hadi kwenye hospitali hiyo
ambapo kweli mrembo huyo alikuwa amelazwa kwa matatizo ya presha ya
kupanda.
Mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mama mdogo wa Angel alimjia juu
paparazi wetu akidai yeye ndiyo chanzo cha mwanaye huyo kupandwa na
presha ghafla, akamtimua asimuone mgonjwa.
MAZUNGUMZO YA BAADAYE
Siku iliyofuata, paparazi alibahatika kuzungumza na Angel ambaye aliweka wazi mambo yake kuhusu picha hizo kama ifuatavyo:
“Mimi nataka kusema kwamba picha nimeziona, nazifahamu kweli ni mimi.”
Paparazi: “Ni kweli ulipigwa ukiwa na mheshimiwa Komba?”
Angel: “We jua tu kwamba picha nazijua. Zilipigwa na simu ya LG.”
Paparazi: “Alipiga nani?”
Angel: “Nimesema nazifahamu.”
Paparazi: “Hiyo simu ni ya nani?”
Angel: “We wa nini?”
Paparazi: “Okey, mheshimiwa Komba unamfahamu?”
Angel: “Namfahamu ndiyo.”
Paparazi: “Ni nani wako?”
Angel: “Nimekwambia namfahamu.”
Paparazi: “Sasa mbona mheshimiwa Komba anasema picha zimetengenezwa?”
Angel: “Mimi sijui sasa.”
ANGEL ATAKIWA KUTIA TIMU GLOBAL
Baada ya mazungumzo hayo, paparazi alimtaka msichana huyo kufika kwenye ofisi za magazeti ya Global ambapo alikubali.
Hata hivyo, baadaye alisema amebatilisha baada ya baba yake kuingilia
kati sakata la picha hizo akidai yeye ndiye atakuwa msemaji mkuu.
Habari za chini kwa chini zilidai kwamba, kusita kuweka miguu kwa Angel
kwenye ofisi za Global kulitokana na zuio la mheshimiwa mmoja ambaye
alimchimba mkwara kwamba asitoe ushirikiano wowote na vyombo vya habari.
MASWALI MUHIMU
Maneno ya Angel na mheshimiwa Komba yanapingana. Mmoja anasema picha
zilitengenezwa, mwingine anazitambua na zilipigwa kwa simu ya LG, nani
mkweli? (endelea kufuatilia Magazeti Pendwa ya Global Publishers).
ANATAJWA PAULINA
Mbali na kupishana kwa maneno ya wawili hao, mwanamke mmoja aliyetajwa
kwa jina moja la Paulina anatajwa kuwa nyuma ya sakata hilo.
Mwanamke huyo anadaiwa wakati fulani kuingia kwenye mzozo na Angel na
akaja kudai ameipata simu yenye picha za mrembo huyo na mheshimiwa bila
kujulikana alikoipata. Je, aliipata kwa Angel au mheshimiwa Komba?
(endelea kusoma magazeti ya Global).