0digg
Neville Meena, Dodoma naGasper Andrew, Singida
MBUNGE wa Ubungo (Chadema), John Mnyika jana alihojiwa na polisi kutokana na vurugu zilizosababisha kifo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kata ya Ndago, wilayani Iramba, Yohana Mpinga (30).Mnyika ni mmoja wa viongozi wa Chadema ambao walihutubia mkutano huo uliofanyika katika Jimbo la Singida Magharibi.Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Robert Manumba alieleza nia ya jeshi hilo kutaka kumhoji Mnyika kuhusu tukio hilo, lakini hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hili akishauri aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.
Mnyika aliyekwenda Singida kuitikia wito wa polisi, alihojiwa na kikosi maalumu cha maofisa wa jeshi hilo kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam, ambao wako mkoani humo kuchunguza matukio ya vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha kifo cha kada huyo wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida jana, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kuwa, Mnyika alifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida jana saa 7.45 mchana kuitikia wito uliotumwa kupitia Ofisi za Bunge.
Makene alimnukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa akisema, Mnyika anapaswa kuhojiwa na kikosi maalumu cha maofisa wa Polisi kutoka Dar es Salaam ambacho kwa wakati huo, kilikuwa Ndago kufanya upelelezi wa kitaalamu zaidi kuhusiana na mauaji ya Yohana.
“Kutokana na kauli hiyo, hivi sasa Mbunge Mnyika amepumzika hadi hapo saa kumi jioni, atakapohojiwa na hicho kikosi maalumu, anahojiwa kuhusu nini, hiyo ni siri hakuna anayefahamu,” alisema Makene.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyika alisema akiwa katika Ofisi ya RPC Sinzumwa alihoji iwapo alitakiwa kuhojiwa kama mtuhumiwa au shahidi.“Jibu la RPC ni kwamba ni mahojiano ni ya kawaida tu, nilihoji sababu Mwita (Mwikwabe) aliambiwa kwamba ni mahojiano ya kawaida, lakini baadaye aliwekwa ndani na kupandishwa kizimbani,” alisema Mnyika.
Gazeti hili lilipowasiliana na Makene jana saa 11.30 jioni, alisema walikuwa bado hawajaitwa kwenda kuhojiwa na badala yake polisi waliwataka kuendelea kusubiri kwa kuwa maofisa waliokwenda Ndago walikuwa wamekwama njiani.
Bungeni Dodoma
Mapema jana asubuhi kulikuwa na habari kwamba Mnyika amekamatwa na polisi akiwa mjini Dodoma anakohudhuria vikao vya Bunge la Bajeti, lakini ikabainika kwamba alikwenda mwenyewe Singida kuitikia wito wa polisi.
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge wa Chadema, John Mrema alisema jana mjini Dodoma kuwa, Mnyika alikwenda Singida kuitikia wito wa polisi ambao walimwita kupitia Ofisi ya Spika wa Bunge.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema kuwa, juzi Bunge lilipokea barua kutoka polisi mkoani Singida ikitoa wito kwa Mnyika kwenda kufanyiwa mahojiano kuhusiana na vurugu zilizotokea katika mkutano mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Kweli polisi walifika hapa wakawasilisha barua wakiomba kwamba Mnyika afike Singida kwa ajili ya kuhojiwa na sisi baada ya kuwasiliana na Spika tulimwarifu na ninaamini leo (jana) atakuwa amekwenda huko,” alisema Joel jana.
Chadema walalama
Wakati Mnyika akiendelea kusubiri kuhojiwa, Chadema jana kililalamikia polisi kutochukua hatua dhidi ya watu waliowafanyia fujo kwenye mkutano wao.
“Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa Singida alifungua kesi dhidi ya baadhi ya watu waliokuwa wakiongoza vurugu za kuvuruga mkutano, lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa, tumeuliza RPC anasema eti analifuatilia,” alisema Makene.
Alidai kwamba vurugu hizo zilifanywa na watu wachache na kwamba majina yao yaliwasilishwa polisi, lakini hakuna hatua zozote zilizochukukiwa.
“Kutoka eneo ambalo tulikuwa tukifanyia mkutano mpaka hapo kituo cha polisi kilipo ni kama hatua 25 au 30 hivi na jalada tulifungua na majina ya watu 12 waliotufanyia fujo tuliyawasilisha,” alisema na kuongeza:
“Lakini tulipowauliza polisi kama kuna hatua zozote walizowachukulia watuhumiwa hao, tumejibiwa kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye ameshakamatwa mpaka sasa.”