Tuesday, September 24, 2013

MASIKINI BABA WEMA APOOZA UPANDE MMOJA


Stori: Imelda Mtema
MasIkini! Baba mzazi wa Miss Tanzania mwaka 2006 ambaye pia ni staa mkubwa wa filamu, Wema Sepetu, mzee Isaac Abraham Sepetu yupo kitandani akiwa amepooza upande mmoja wa mwili wake.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi (kulia), akimjulia hali mzee Isaac Abraham Sepetu.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, mwishoni mwa wiki iliyopita aliiwakilisha serikali kwenda kumjulia hali mzee huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo visiwani Zanzibar na balozi katika nchi mbalimbali ambaye yupo nyumbani kwake Sinza-Mori, Dar.
Katika hali ya kusikitisha, mama mzazi wa Wema, Mariam Sepetu, aliliambia gazeti hili ambalo lilikuwa limeongozana na Nchimbi kuwa, mume wake alipatwa na ugonjwa huo akiwa kazini Zanzibar, ingawa kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na kisukari.
Alisema baada ya kupata taarifa za ugonjwa huo, familia ilipanda ndege kutoka Dar kuelekea Zanzibar ambako walimchukua na kumpeleka Hospitali ya TMJ ya jijini Dar, alikolazwa kwa muda wa wiki tatu kabla ya kuruhusiwa.
“Ingawa bado amepooza, lakini kwa sasa hali yake ni afadhali kuliko alivyokuwa mara ya kwanza,” alisema mama huyo aliyedai kuwa mumewe ni mgonjwa kwa mwezi mmoja sasa na kwa kipindi chote hicho, amekuwa akifanyiwa kila kitu.
WASIFU MFUPI WA MZEE SEPETU
Balozi Sepetu aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje mnamo miaka ya 1970 wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Kambarag Nyerere.  Vilevile, aliwahi kuwa balozi nchini Urusi tangu mwaka 1982 wakati wa utawala huohuo wa Nyerere.
Pia, Machi 27, mwaka huu, Balozi Sepetu aliteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dr Mohammed Shein,  kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitegauchumi ya Zanzibar (ZIPA).



Love to hear what you think!