Friday, September 27, 2013

KIFO TATA, KIONGOZI CCM AFIA KWA MGANGA


Stori: Hamida Hassan na Gladness Mallya
MJUMBE wa Serikali ya Mtaa wa Michungwani, Kimara King’ong’o jijini Dar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni kiongozi wa umoja wa wazazi, Seleman Hashim Ndege amefariki dunia nyumbani kwa mganga wa kienyeji ‘Sangoma’, Veronica Kasumen ‘mama Misingo’ na kifo chake kuacha utata, Ijumaa lina habari kamili.
Marehemu Seleman Hashim Ndege enzi za uhai wake.
Akizungumza kwa uchungu mke wa marehemu, Mwajuma Ally amesema kuwa siku ya tukio (Jumamosi iliyopita) mume wake aliamka asubuhi saa 12 na kwenda kusambaza vipeperushi vya kazi zake za serikali ya mtaa.
Mwajuma alisema ilipotimu saa tisa alasiri, alifuatwa na mama Misingo na kumwambia kuwa mume wake amefariki dunia nyumbani kwake na kumtaka waende kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Tumbi, Kibaha.
“Nilishtuka sana kwa kuwa mume wangu hakuwa akiumwa chochote, niliambatana na mama Misingo kwenda nyumbani kwake,” alisema Mwajuma kwa unyonge.
Sehemu ya waombolezaji wakiwa msibani.
Mke huyo aliendelea kudai kwamba alipotoka nje alikutana na gari la  Kituo cha Polisi cha Mbezi Kwa Yusuf waliomwamuru kuingia ndani ya gari hilo aina ya Land Rover ‘Difenda’ huku wakimuuliza kama amemuona mume wake.
“Kilichonishtua ndani ya gari kulikuwa na wanaume wengine wawili wakanionesha mwili wa mume wangu ukiwa tayari umeshavalisha sanda bila ya kunishirikisha,” aliendelea kusema Mwajuma.

Jeneza lenye mwili wa marehemu.
Mke huyo alisema kuwa alimhoji mama Misingo kilichotokea, naye akamwambia kuwa mumewe alifika kwake kwa lengo la kumuona mtoto wake ambaye alianguka na pikipiki lakini ghafla akaanguka na kuaga dunia mara baada ya kuomba kuingia msalani.
“Tulienda mpaka Hospitali ya Tumbi ambapo mwili ulihifadhiwa kisha tukarudi nyumbani,” alimaliza mke wa marehemu huku akisema kuwa amebaki na utata juu ya kifo cha mumewe.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Michungwani ambapo marehemu alikuwa akiishi, Fadhili Mzee Jakaya alisema alishtushwa na taarifa za kifo hicho na kuzifuatilia.
“Mimi na wenzangu tulienda Kituo cha Polisi cha Mbezi lakini tulishangaa kukuta mganga huyo (mama Misingo) ameandikisha kuwa ni mkazi wa Kibamba na aliyefariki ni kaka yake aliyefika nyumbani kwake kumuona mpwa wake ndipo alipoanguka chooni, hicho kilitushangaza,” alisema.
Jakaya alisema kitendo cha mganga huyo kudanganya eneo analoishi na udugu wake na marehemu kiliwafanya waamini kuwa kulikuwa na kitu nyuma ya pazia.
“Tunasikia Ndege alifariki saa tatu asubuhi, imekuwaje wamekaa naye hadi saa tisa jioni, haya kama si maajabu ni nini? Pia kwa nini wamvalishe sanda?  Hapa kuna sababu zitajulikana tu,” alisema Jakaya.
Wananchi wa Michungwani walijikusanya na kwenda nyumbani kwa mama Misingo na kumkuta akiwa na mumewe ambapo walimhoji kuhusu maelezo tata aliyoyatoa kituo cha polisi.
Hata hivyo, viongozi wa serikali ya mtaa walitoa taarifa polisi ambao walifika nyumbani kwa mganga huyo baada ya nusu saa na kuondoka naye.
Habari zilizopatikana kutoka kwa majirani zinadai Ndege alifika nyumbani kwa mama Misingo na kutibiwa kwa kupewa dawa lakini cha ajabu akafariki dunia.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa King’ongo anapoishi mama Misingo, Demetrius Mapesi amesikitishwa na  kitendo hicho na kusema iwapo vipimo vitabaini kuwa dawa aliyokunywa marehemu ni sumu watachukua hatua kali.
Waandishi wetu walifika nyumbani kwa mama Misingo na kuzungumza na watoto wake, ambapo mmoja wao alisema kuwa, marehemu alifika nyumbani kwao saa tatu asubuhi kwa lengo la kumuona kaka yao aitwaye George ambaye alikuwa mgonjwa.
“Baada ya muda aliomba kwenda chooni na kukaa huko kwa muda mrefu, mama akamsikia akikoroma ndipo akaniambia nivunje mlango nimtoe.
“Nilifanya hivyo, tulikuwa na mama na mzee mmoja (jina linahifadhiwa) tulijaribu kumvua nguo na kumwagia maji lakini alikuwa tayari ameshafariki dunia, mama akapiga simu kuwaita polisi,” alisema mtoto huyo.
Naye jirani mwingine wa mama Misingo aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema hawakupewa taarifa za mtu kuanguka chooni na alipoliona gari la polisi limewabeba alihoji na kuambiwa kuwa hakukuwa na tatizo lolote. 
Baada ya kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Tumbi, mwili wa marehemu uliagwa nyumbani kwake Kimara Michungwani kisha kusafirishwa kwenda Mtwara kwa ajili ya mazishi ambapo mtaani vilio vilitawala kila kona wakati wa kuuaga mwili.
Bado wakazi wa Kimara Michungwani wanasubiri taarifa ya daktari ili kujua kilichosababisha kifo cha Ndege.
Love to hear what you think!