Sunday, September 29, 2013

"ACHENI KUMLAZIMISHA RAIS KIKWETE KUSAINI MUSWADA"....ZITTO


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kabwe Zitto amewaonya baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani na chama tawala kuacha kumlazimisha Rais Kikwete kutekeleza maoni yao binafsi kuhusu Muswada wa Sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011.
Badala yake amewataka wanasiasa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kutambua kuwa Katiba ni uhai wa Mtanzania hivyo kurejea katika meza ya mazungumzo kwa pande zinazovutana kuhusu nini kifanyike ili kuona namna ya kupata muafaka wa suala hili.
Zitto katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, alieleza kuwa ingawa kumekuwa na sintofahamu, vuta nikuvute kuhusu muswada huo, bado kuna nafasi kama taifa kukaa na kukubaliana na kuongeza kuwa kwa hali ilivyo nafasi hiyo ipo mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
“Rais ana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama kutoridhia sheria hiyo.
“Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo, kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi,” alisema Zitto.
Zitto alisema kwa takriban wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada huo, jambo lililoweka historia mbaya wakati wa mjadala wa suala hilo bungeni kulikochangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo jambo ambalo halileti muafaka wa kitaifa.
Alisema masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na kuzungumza.
“Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa. Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na Katiba mpya ya wananchi,” alibainisha Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema.
Aidha, alisema lipo kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata kile kinachodhaniwa kuwa ni Katiba bora huku kundi la Wabunge ambao chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge, jambo ambalo halihusiani kabisa na kupata Katiba mpya. Zitto alikumbusha kuwa Chadema iliwahi kupendekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na kadhalika.
Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.
Alisema changamoto kubwa ya siasa za Tanzania ni kelele ambapo alidai wanasiasa hawazungumzi masuala yanayohusu uhai wa Taifa, bali kila chama kinakuwa na misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania.
“Vyama vya upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo, badala ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno,” alieleza Zitto.
Alisema taifa linajengwa kwa mwafaka hivyo alielekeza nafasi hiyo kwa Rais Kikwete kwamba atumie mamlaka yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge.
“Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote”, alifafanua Zitto.
Naye Regina Kumba anaripoti kuwa viongozi wa vyama vya upinzani wamekutana na msajili wa vyama vya Siasa, Francis Mutungi na kumueleza sababu za kutaka Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada wa Mabadiliko ya katiba.
Aidha wamesema watashawishi wananchi kupinga muswada huo iwapo rais atausaini. Viongozi hao wa CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR-Mageuzi, wamesema pia walimueleza kilichotokea Bungeni Mkutano uliopita kwa wabunge wa vyama vya upinzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kukutana na msajili, Msemaji wa Chadema na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema walikutana na Mutungi kwa nia ya kumueleza nia yao.
“Tuliamua kuja kwa msajili kumueleza kilichotufanya kuondoka katika Bunge lililopita na kwanini tumeamua sasa kwenda kwa wananchi kufanya majadiliano baada ya yaliyotokea Bungeni ili kupata hatima ya katiba yetu.”
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema ujio wao kwa msajili wa vyama vya siasa ni kumueleza kilichojiri katika mchakato wa katiba ambao toka awali haukwenda vizuri kutokana na ushiriki wa Zanzibar kuwa mdogo.
“Tumemjulisha kwa nini tumekuwa na msimamo huu kuwa ikiendea kusainiwa rasimu hiyo kutakuwa hakuna maana ya ushiriki wetu hivyo hatutashiriki tena kwa sababu Katiba ni ya Watanzania na sio ya chama kimoja,” alisema Lipumba.


Love to hear what you think!