Tuzo aliyojishindia mwanamitindo Flaviana Matata.
---
MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata ameendelea 
kung’ara kimataifa baaada ya kushinda tuzo ya Nigeria’s Next Super Model
 na kuwa mwanamitindo bora barani Afrika wa mwaka 2012 (Africa’s Most 
Outstanding Model 2012).
Tuzo hiyo utolewa kwa wanamitindo ambao bado wanailetea sifa Afrika
 kimataifa na Flaviana amekuwa katika chati ya juu. Mwaka jana Desemba, 
 Flaviana alishinda tuzo nyingine  ya uwanamintindo bora kutoka kwa 
diaspora ya Waafrika.
Flaviana ambaye kwa sasa  anaishi na kufanya kazi ya uanamitindo 
New York nchini Marekani kupitia shirika la Wilhelmina Models, mpaka 
sasa ameweza kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na umahiri wake 
katika maonyesho ya mavazi.
Tangu ashinde taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2007, Flaviana 
amekuwa aking’ara katika kona zote za dunia na hasa baada ya kumaliza 
katika nafasi ya sita katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe, 
huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza.
Ameweza kushiriki katika maonyesho ya mavazi mengi Ulaya na Amerika
 huku akitoa misaada mingi kwa Watanzania wenzake ambao wamekuwa na 
ndoto ya kufika mbali katika fani hiyo.
Kwa sasa Flaviana anaendesha taasisi yake, Flaviana Matata 
Foundation ambayo inasomesha watoto wa kike 16 na mwaka jana alitoa 
msaada wa vifaa vya kuokoa maisha kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzama 
kwa meli ya MV Bukoba huku ikiwa kumbukumbu ya kifo cha mama yake mzazi 
katika ajali hiyo ya mwaka 1996.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Compass Communication Tanzania 
Limited, Maria Sarungi Tsehai alisema kuwa wamejisikia faraja sana kwa 
kumvumbua mwanamitindo huyo ambaye kwa sasa anashika chati ya juu 
Tanzania na nje ya nchi.
Maria alisema kuwa Flaviana amedhihirisha ubora wake na mpaka sasa 
amepitiliza kiwango cha kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake, ndoto 
ambayo alikuwa nayo muda mrefu.


 
