MWANAFUNZI wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Kipwa mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa mwenye miaka minane ameweza kujiokoa yeye na mtoto wa dada yake mwenye umri wa miezi mitano kwa kuogelea hadi ufukweni baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye ziwa Tanganyika.
Manusura huyo aliyefahamika kwa jina moja la Prisca akiwa miongoni mwa wengine 15 walinusurika kufa maji ama kwa kuogelea au kuokolewa alipoona mtumbwi huo ukizama, inadaiwa alipiga mbizi majini akiwa na mtoto huyo mchanga mgongoni mwake na kuweza kuogelea kwa saa kadhaa hadi ufukweni wote wakiwa hai.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kipwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika , Benson Silinjile alithibitisha mkasa huo wa aina yake akisema msichana huyo Prisca alikuwa amempeleka mtoto huyo kupata chanjo katika kituo cha afya kijijini Kapele kwa kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa mgonjwa hivyo alimwomba msaada huo.
Licha ya msichana huyo kuweza kujiokoa yeye na mtoto huyo mchanga kwa kuogelea hadi ufukweni pia nahodha wa mtumbwi huo uliopata ajali hiyo iliyosababisa vifo vya watu 13 wakiwemo wanawake na watoto wenye umri chini ya miaka mitano , Lazaro Sikapote (26) aliweza kuokoa familia yake akiwemo mama yake mzazi Rose Sikapote , mkewe Rakadia Sikazwe na mwanae aliyefahamika kama Nazaro Sikapote.