Rais Jakaya Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan, Omar Bashir, kuhusu kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu, na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.
Rais Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Alimueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini waliohusika ni wahalifu, kusisitiza kuwa lazima watasakwa hadi kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Alimpa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha, ambapo wanajeshi wa Tanzania walienda nchini Sudan kulinda amani na usalama wa wananchi wa Sudan.
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alimpigia Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha, ambao umewatokea Watanzania hao wakati wakitekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi chochote kilichokiri kuhusika na shambulio hilo, ingawa kumekuwa na hali ya kutupiana lawama baina ya vikundi vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano baina ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali, yamesababisha mapigano na uvunjifu mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10 sasa.
Mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.
Mwishoni mwa mwaka jana wanajeshi wanne kutoka Nigeria, waliuawa karibu na El Geneina, Magharibi mwa Darfur, ambapo pia inaelezwa na AU kuwa wanajeshi wapatao 50, wameuawa tangu kikosi hicho cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID), kianze operesheni yake mwishoni mwa 2007.
Taarifa za UN pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania Jumamosi iliyopita, wanajeshi sita wanaolinda amani waliuawa tangu Oktoba mwaka huu, ambapo pia inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000 wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo, kiini cha mgogoro huo inasadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan.
Miili ya maaskari hao saba wa Tanzania, inatarajiwa kuwasili nchini Ijumaa, Julai 19 kwa ajili ya maziko.