Hatimaye siku imetimia, ile siku ambayo kila mja na muungwana
katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya alikuwa akiingoja, usiku wa
tunzo za Kilimanjaro Tanzania, zitaunguruma kuanzia saa moja hadi
kuendelea, Watanzania takriban 32 wanaofanya kazi katika tasnia ya
muziki wanatarajiwa kuondoka na tunzo mikononi mwao leo.
Zaidi ya wasanii 100 wametajwa kuwania tunzo hizi,
na wote wana imani ya ushindi na watakuwa ukumbini leo pamoja na baadhi
ya mashabiki wao, kushuhudia matokeo ya kazi ngumu waliyoifanya katika
msimu uliopita wa muziki wa Tanzania.
Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia kinywaji chake
cha Kilimanjaro, kilichodhamiria kupeleka muziki wa Tanzania katika
kilele cha mafanikio, leo ndiyo mwenyeji wa shughuli husika na wameahidi
usiku wa kihistoria, huku wakiadhimisha mwaka wa 13, wa tunzo hizi
ambazo kila kukicha zinazidi kujizolea umaarufu.
George Kavishe, ni Meneja wa bia ya Kilimanjaro na
amefanya mahojiano na gazeti hili kuhusiana na usiku wa leo na mambo
muhimu makubwa matatu yametajwa katika kuunogesha usiku mwingine wa
tunzo, uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu.
Kwanza, usiku hautakuwa Dar es Salaam peke yake
utakuwa katika mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Dar ambapo katika viwanja
mbalimbali vya Taifa Dar es Salaam, Mabatini Mwanza, na CCM Mkoa kwa
Kilimanjaro kutakuwa na TV kubwa zitakazokuwa zikionyesha moja kwa moja
tukio la utoaji tunzo litakalokuwa likiendelea katika Ukumbi wa Mlimani
City usiku wa leo.
Watazamaji wa mikoani, watashuhudia tunzo hizo kwa
kiingilio cha bia moja tu milangoni, na wakiingia katika viwanja hivyo
watakuta maandalizi mazuri kutoka kampuni ya bia Tanzania, na watakuwa
wakishuhudia onesho lote, pamoja na burudani mbalimbali zitakazokuwa
zinatolewa na waandaaji.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam
watakaopata bahati ya kuhudhuria onesho hilo ambapo kiingilio kitakuwa
Sh 75,000 kwa watu maalumu na kawaida itakuwa Sh20,000.
“Sababu mbili za msingi za kuweka onesho hili
uwanjani, kwanza, ni kutokana ma mfumo wa digitali, ambapo Watanzania
wengi wameshindwa kukabiliana nao kutokana na hali ya kiuchumi, hivyo
tumewapa fursa nyingine ya kushuhudia tunzo, lakini pia tungependa
mashabiki wakae pamoja na kushuhudia tukio hili la kihistoria,”
alisisitiza George Kavishe.
Red Carpert
Hili ni zoezi litakalohusisha mastaa hasa upande
wa mitindo, ambapo picha zitakuwa zikichukuliwa, katika kuperuzi nani
kaja vipi na kavaa nini na alikuwa amesindikizwa na nani.
Hii itakuwa na mtangazaji wake na itakuwa ni kama
sehemu ya kipindi cha TV na kwa habari tulizonazo, ni kwamba mtangazaji
wa Channel O na mdau mkubwa wa burudani, Jokate Mwegelo ndiye atakuwa
mwendeshaji.
Kwa mujibu wa waandaaji, zoezi litachukua kama saa limoja hivi, maana shughuli yenyewe itaanza saa mbili usiku