MAHAKAMA Hakimu ya Mkazi ya Wilaya ya
Mpanda imemhukumu Kassim Lugendo (41) mkazi wa kijiji cha Kambanga
tarafa ya Kabungu kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kumnyonya ulimi
mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13, anayesoma darasa la tano katika
Shule ya Msingi Igalula, bila ridhaa yake.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Chiganga Tengwa alitoa hukumu hiyo jana baada ya kuridhika na ushahidi
uliotolewa mahakamani hapo.
Awali katika kesi hiyo, Mwendesha
Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Ally Mbwijo aliieleza mahakama hiyo kuwa
mshitakiwa Lugendo alitenda kosa hilo Machi 30 mwaka jana, saa sita
mchana akiwa nyumbani kwake.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio mtoto
huyo alikuwa akitoka shuleni akielekea nyumbani kwao ndipo mshitakiwa
alipoona anapita karibu ya nyumba yake ambapo alimwita msichana huyo na
kisha alimwingiza kwa nguvu nyumbani kwake.
Mbwijo aliiambia mahakama kuwa, baada ya
mshitakiwa kumwingiza ndani ya nyumba yake msichana huyo, alianza
kumnyonya ulimi kwa nguvu huku akimtomasa sehemu za siri kwa vidole.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa wakati
akimfanyia uovu huo, mtoto huyo alikuwa akiomba msaada kwa kupiga kelele
muda ambapo majirani walifika eneo la tukio na kumkuta mshitakiwa akiwa
ameshaanza kumvuta mtoto huyo sketi yake ya shule.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulileta mahakamani hapo mashahidi watatu na mshitakiwa hakuwa na shahidi yeyote.
Akijitetea, Lugendo aliiomba mahakama
isimpe adhabu kwa kile alichokieleza kuwa yeye ana familia ya watoto
saba na wazazi wake wote wawili ni walemavu, hivyo ana watu wengi
wanaomtegemea.
Hata hivyo, Hakimu Chiganga alisema
kitendo alichokifanya mshitakiwa ni cha kinyama na hatari kwani kina
weza kumsababishia mtoto huyo ugonjwa wa ukimwi. Alimtia hatiani na
kumwadhibu kifungo cha miaka kumi jela