Tuesday, March 12, 2013

MWALIMU AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI

Na Waandishi Wetu, Njombe
HAIWEZI kuwa hasira, wala haiingii akilini kuwa mwendesha pikipiki asipovaa kofia ngumu (helmet), adhabu yake inaweza kuwa kifo cha kumiminiwa risasi.
Askari wa jeshi la polisi, PC Jose Msukuma, anatuhumiwa  kumuua Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kitulo wilayani Makete, Castor Kawambwa kwa kumpiga risasi mgongoni.
Habari zinadai kwamba Jose alimtwanga risasi Mwalimu Kawambwa baada ya kubaini kuwa alikuwa anaendesha pikipiki bila helmet.
Tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita wilayani Makete, Njombe.
ILIVYOKUWA
Uchambuzi kuhusu namna tukio lilivyotendeka, unabainisha kuwa Jose alimsimamisha Mwalimu Kawambwa, alipokaidi amri ndipo akamtwanga risasi iliyotoa uhai wake.
“Ni tukio ambalo limetushangaza sana. Inawezekanaje polisi afanye vitendo vya namna hii?” kilihoji chanzo chetu na kuongeza:
“Haiingii akilini kwamba adhabu ya mwendesha pikipiki inaweza kuwa kifo cha kupigwa risasi eti kwa sababu alisimamishwa, akagoma kusimama.”

RPC NJOMBE AANIKA KILICHOPO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Peter Kaiza alisema kuwa Mwalimu Kawambwa alipigwa risasi na Jose jirani na Benki ya NMB, Tawi la Makete.
“Mwalimu huyo alikuwa anakwenda kupata huduma za kibenki kupitia mashine ya kutolea pesa, ATM akiwa na pikipiki ndipo alipoamriwa na askari huyo asimame kabla ya kukutwa na umauti,” alisema Kamanda Kaiza.
Aliongeza, kifo cha mwalimu huyo kilitokana na kukaidi kusimamishwa na askari baada ya kutovaa kofia aina ya helmet na kutaka kumgonga (askari), ndipo alipompiga risasi.
Akaongeza kuwa upelelezi juu ya tukio hilo umeshaanza kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zinazostahili.
MKURUGENZI HALMASHAURI ANENA
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Idd Nganya ambaye ndiye mwajiri wa marehemu, amesema kuwa maiti ilisafirishwa na kupelekwa Mbeya kwa mazishi.
RIPOTI YA DAKTARI
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Makete, Dk. Michael Gulaka alisema kwamba walipokea mwili wa marehemu ukiwa na majeraha ya risasi mgongoni na kwamba wakati huo alikuwa amekwisha fariki duni


Love to hear what you think!