Sehemu ya ukuta iliyobomoka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.
Wasamaria wema wakijaribu kumwokoa kijana aliyeangukiwa na ukuta kwa kufukua kifusi kwa mikono.…
Sehemu ya ukuta iliyobomoka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.
Wasamaria wema wakijaribu kumwokoa kijana aliyeangukiwa na ukuta kwa kufukua kifusi kwa mikono.
MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Kwakilosa
katika Manispaa ya Iringa Daniel Yona (15) amefariki dunia baada ya
kuaungukiwa na ukuta wa uwanja wa Samora wakati akijaribu kupita mlango
wa panya ili kwenda kushuhudia tamasha la Mtikisiko 2012.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 2 mwaka huu wakati
wapenda burudani katika mkoa wa Iringa walipofika katika uwanja huo
kushuhudia onyesho kubwa la Mtikisiko 2012 ambalo lilikuwa limepambwa na
wasanii mbali mbali wakiongozwa na mkongwe Juma Nature na Profesa J.
Wakielezea kilichomkuta mwanafunzi huyo baada ya mashuhuda walisema
kuwa mwanafunzi huyo na wenzake waliacha kupita katika mlango wa
kawaida kwa kulipia kiingilio halali kilichowekwa na badala yake aliamua
kupita gizani na kupanda ukuta huo wa uwanja wa Samora ili kuweza
kuingia ndani ya uwanja huo kuona tamasha la Mtikisiko.
Hata hivyo mmoja kati ya mashuhuda ambae hakupenda kutajwa jina
lake hapa alisema kuwa kabla ya mwanafunzi huyo kupanda ukuta huo kuna
vijana kama 20 ambao walifanikiwa kupita eneo hilo bila kulipa kiingilio
na baada ya kufanikiwa kupita walianza kupigiana simu huku baadhi ya
vijana wa kitanzini wakiwatoza vijana hao wanaoruka ukuta kiingilia cha
shilingi 1000 hadi shilingi 500 .
"Ujue hapa vijana wa kihuni kutoka Kitanzini walikuwa wamejipanga
hapa na kufanya ufisadi wa kuwatoza watu kiingilio bila wahusika wa
Tamasha hilo kujua kinachoendelea .....hivyo hata huyo mwanafunzi
alikuwa ni mmoja kati ya wavamizi wa Tamasha hilo kwa kupita njia ya
panya ili kuingia ndani ya uwanja huo"
Pia alisema ukuta huo ulionyesha kuzidiwa nguvu kutokana na ubovu
wa ukuta wenyewe kuwa ni mbovu na ulikuwa umeungwa kienyeji katika eneo
hilo.
Aidha alisema baada ya vijana zaidi ya watano kupanda eneo hilo la
ukuta ambalo lipo upande wa kushoto mwa uwanja huo wa uwanja ukuta huo
ulionyesha kuyumba na kupelekea vijana wengine kuruka na kumwacha
mwanafunzi huyo ambae tayari alikuwa ameingiza mguu mmoja ndani ya
uwanja na mguu wa pili ulikuwa nje.
Alisema baada ya ukuta huo kuanguka na kumfunika walifanikiwa
kumwokoa akiwa hai na kumkimbiza Hospitali ya mkoa wa Iringa ambako
asubuhi ya siku ya pili ya Desemba 2 majira ya saa 5 asubuhi alifariki
dunia.
Hata hivyo askari polisi waliokuwepo eneo hilo la tukio
walimthibitishia mwandishi wa mtandao huu kuwa ni kweli kijana huyo
amefariki dunia japo wao si wasemaji wa jeshi la polisi na kudai kuwa
chanzo ni kijana huyo mwenyewe kutaka kupita mlango wa panya na kuacha
kupita mlangoni ambako watu wote walikuwa wakipita bila kupata matatizo
yoyote.
Hata hivyo uchunguzi wa mtandao huu unaonyesha kuwa kifo cha
mwanafunzi huyo kimesababishwa na mwanafunzi mwenyewe kutokana na kutaka
kupita njia ya panya na kuacha mlango kwani iwapo angetumia njia sahihi
kuingia uwanjani yawezekana kifo kisingeweza kutokea.
CHANZO: FRANCIS GODWIN BLOG