Thursday, August 2, 2012

AFISA ELIMU ADAKWA AKINYWA POMBE SAA ZA KAZI

WAKATI mgomo wa walimu ukiendelea kufukuta nchi nzima na Serikali ikijaribu kuuzima, Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Korogwe, anadaiwa kukamatwa kwa tuhuma za kunywa bia muda wa saa za kazi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Chanzo chetu cha habari kimesema kwamba ofisa elimu huyo alikamatwa saa 5 asubuhi kwenye baa moja maarufu iliyopembezoni mwa barabara kuu akiwa anakunywa pombe ambapo askari walimkamata na kumfikisha kituo kikuu cha polisi wilayani hapa.

Kukamatwa kwa ofisa huyo kumekuja  siku moja tangu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo kuamua kuingia darasani katika shule tatu tofauti na kuamua kufundisha wakati mgomo wa walimu ukiendelea.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Korogwe Julai 31, mwaka huu  alilazimika kuingia darasani kwenye Shule za Msingi ya Mbeza ,Bagamoyo na Manundu akifundisha somo la hisabati , ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha wanafunzi kusoma baada ya walimu wao kugoma.

Jana, Gambo akizungumzia tukio la kukamatwa kwa ofisa elimu huyo, alisema lilitokana na agizo lake baada ya kupokea taarifa kupitia meseji ya simu ya mkononi kutoka kwa wananchi kwamba ofisa huyo anakunywa pombe baa.

Sehemu ya ujumbe huo wa simu ambao mwananchi imefanikiwa kuupata inasema”Inasikitisha ofisa elimu sekondari Wilaya ya Korogwe yuko Blue Palm nyuma ya stendi anakunywa pombe saa hizi huku walimu wakiwa wamegoma? hii ni Serikali gani? njoo umuone”ulisema ujumbe huo wa simu ya mkononi aliyotumiwa DC.

Akithibitisha tukio hilo mkuu huyo wa wilaya alisema:“Taarifa za ofisa elimu huyo ninazo, mimi ndiye niliyeagiza akamatwe baada ya kupata taarifa kuwa ameonekana anakunywa pombe muda wa kazi”alisema mkuu wa wilaya.

Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kwamba baada ya kukamatwa mwalimu huyo aliagiza afikishwe hospitalini ili kupimwa lengo likiwa kuweza kubaini kiasi cha alkoho kilichomo kwenye mwili wake ili hatua za kinidhamu za kiutumishi zichukuliwe dhidi yake.

Aidha mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba baada ya vipimo hivyo kufanyika na ofisa huyo kuibainika kwamba alikuwa na kilevi kwenye mwili wake hatua za kiutumishi zitachukua nafasi yake ambapo pia mhusika anaweza kufutwa kazi kwa kosa hilo.
“Nimeagiza baada ya kukamatwa ofisa huyo afikishwe hospitalini ili kupimwa kama kwenye mwili wake kuna kilevi,na endapo itabainika hatua kali za kinidhamu na zile za kisheria hazitasita kuchukuliwa dhidi yake”alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipotafutwa ili kuzungumzia sakata hilo simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila ya majibu ingawaje awali alisema atafuatilia na kwenye wilaya husika na kutoa taarifa


Love to hear what you think!