Na Gladness Mallya
JUMAPILI ya Julai 22, mwaka huu ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa msanii wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja, staa huyo alisheherekea siku yake hiyo kwa majonzi akiwa katika Gereza la Segerea jijini Dar huku vilio vikitawala.
‘Bethdei’ hiyo ilifanyika Jumapili ambapo baadhi ya wasanii walifika katika gerezani kwa ajili ya kumpelekea zawadi mbalimbali huku wakimwimbia Kajala wimbo maarufu wa ‘Happy Birthday’ wakati staa huyo akiwa nyuma ya nondo.
Baadhi ya watu waliofika gerezani hapo kwa ajili ya kuungana naye katika kusheherekea ni pamoja na mtoto wake Paula, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, Bilaly Mashauzi pamoja na Jeniffer Pemba.
JENIFFER AKABIDHI KEKI
Dada huyo ambaye ni rafiki wa karibu na Kajala ambaye pia ndiye mwenye jukumu la kumpelekea chakula kila siku, Jumapili iliyopita aliandaa keki ya nguvu pamoja na zawadi nyingine kwa ajili ya sherehe ya Kajala, bitu hivyo vilipokelewa na askari wa magereza na kukaguliwa kisha kufikishwa kwa mlengwa.
LULU AJUMUIKA
Baada ya muda mfupi staa mwingine anayetajwa kwenye kifo Steven Kanumba Elizabeth Michael ‘Lulu’ naye alijumuika na Kajala kusimama nyuma ya nondo kwa ajili ya kusheherekea bethdei hiyo pamoja na kuwasalimia watu waliofika ambapo wote walionekana kufarijika na ujio wao.
VILIO VYATAWALA
Hata hivyo, tofauti na ilivyotegemewa kwani vilio vilichukua nafasi gerezani hapo kutokana hali ilivyokuwa kwani Kajala na Lulu hawakuweza kuungana na wapendwa wao kusheherekea pamoja kutokana na sheria za Jeshi la Magereza kutoruhusu tendo hilo.
SHILOLE ALALAMA
Kwa upande wake, Shilole mbali na kushiriki kuangusha kilio lakini alikuwa akilalamika kwamba yupo katika wakati mgumu na haoni raha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kuwa mwaka jana aliwaalika Kajala na Lulu wakala futari pamoja nyumbani kwake.
“Sina budi kuwaombe dua katika mfungo huu wa Ramadhan ili Mungu awajalie waweze kutoka na tuungane tena kama zamani,” alisema.