Wednesday, June 3, 2015

BLATTER AJIUZULU FIFA


Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter.
Zurich, Uswis
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter, jana alijiuzulu cheo chake kutokana na kashfa ya rushwa iliyolikumba shirikisho hilo.Blatter alitangaza kujiuzulu jana jioni zikiwa ni siku nne tangu alipochaguliwa kwa mara ya tano kuiongoza Fifa.
Alitangaza uamuzi huo kwenye makao makuu wa Fifa mjini Zurich akiwa ametumikia cheo cha urais kwenye shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka 17.
“Nimekuwa nikijituma sana kwa kipindi changu chote nilichokaa kwenye taasisi hii kubwa duniani, maisha yangu ni soka na ninaupenda sana mchezo huu.“Nilikuwa nataka kufanya kila kitu kizuri kwenye taasisi hii kubwa, lakini labda sasa niseme kuwa nimeamua kujizulu wadhifa wangu wa urais wa Fifa kutokana na kashfa hii ya rushwa ambayo imetukumba.
“Nataka kuwashukuru wale wote waliokuwa wananiunga mkono kwa kipindi chote ambacho nilikuwa rais wa Fifa, lakini pia natakiwa kuwashukuru wale ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha soka linakuwa,” alisema Blatter.
Kwa takribani wiki sasa, Fifa imekuwa ikilaumiwa na wadau mbalimbali baada ya kuibuliwa kwa tuhuma za rushwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) zinazowahusu maafisa zaidi ya 14 wa shirikisho hilo.Madudu zaidi yanatarajiwa kuibuliwa katika sakata hilo la aina yake katika historia ya mpira wa miguu duniani.
Blatter, 79, sasa amesema kuwa mkutano mkuu wa Fifa unatakiwa kukaa haraka inavyowezekana ili kuitisha uchaguzi mkuu na achaguliwe rais mwingine.Awali mkutano mkuu ulikuwa ukitarajiwa kufanyika Mei 13, mwakani nchini Mexico, lakini sasa inaaminika kuwa mpaka Desemba mwaka huu shirikisho hilo tayari litakuwa na rais mpya.
Hata hivyo, pamoja na kujiuzulu kwake bado kuna kashfa nyingine inachunguzwa jinsi nchi zilivyopewa nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 ikiaminika kuna rushwa ilitembezwa.




Love to hear what you think!