Thursday, December 12, 2013

SAUZI YAJAA MSIBA WA MANDELA

Wanajeshi wakiwa wameubeba mwili wa hayati Mandela kuelekea ofisi za serikali jijini Pretoria.
Mwandishi Wetu na Mitandao
MAOMBOLEZO ya kifo cha aliyekuwa rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini, Nelson Mandela yanaendelea, kubwa kuliko ni nchi hiyo yenye kilomita za mraba 2,798 kufurika waombolezaji kutoka pande zote za dunia na hivyo, hakuna pa kukanyaga na hali hii ni mwanzo na mwisho!
Nelson Mandela.
Habari kutoka jijini Johannesburg nchini humo zinasema, msiba wa Mandela umebadilisha ghafla hali ya maisha ya raia wa nchi hiyo.
HOTELI HAZINA NAFASI
Hoteli nyingi, hasa katika Miji ya Pretoria na Johannesburg (alikofia Mandela), nyumba za kulala wageni, hoteli na sehemu nyingine zenye kuhifadhi watu zimejaa baada ya wateja kukodi kwa muda wote wa msiba hadi mazishi.
Wageni wanaoingia nchini humo kwa ratiba zao za kabla ya kifo wamekuwa wakipata tabu sehemu za kulala, wengine kugeuza wanakotoka.
Familia ya marehemu Mandela ikifuatilia ibada ya kumbukumbu.
Baadhi ya wenyeji waishio nchini humo wamewasiliana na ndugu zao wanaotaka kwenda, kusitisha safari ili kupisha shughuli za mazishi yatakayofanyika Desemba 15, mwaka huu.
BIDHAA BEI JUU
Licha ya kwamba kipato cha kawaida kwa wananchi wake ni cha chini, bei ya bidhaa, hasa vyakula imepanda na wafanyabiashara wengi wanaitumia fursa hiyo kujineemesha.
Rais wa Marekani, Barrack Obama akiwapungia maelfu ya wananchi waliohudhuria ibada ya kumkumbuka Mandela katika Uwanja wa FNB, Soweto, Afrika Kusini.
MIPAKA HAIPITIKI KAMA ZAMANI
Tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kifo cha Mandela ambapo wengi waliweza kuingia nchini humo bila kubanwa na ukaguzi wa kina, kwa sasa ulinzi umeimarishwa ambapo kila muingiaji anaulizwa maswali mengi, hasa yanayohusu usalama.
MAGAIDI WATUPIWA MACHO ZAIDI
Usalama nchini humo tangu kutokea kwa kifo cha Mandela umekuwa ukiwatupia macho zaidi magaidi wa kimataifa ambao wanaweza kutumia mwanya wa maombolezo kupenya na kusababisha maafa.
Baadhi ya waombolezaji.
GRACA MACHEL, WINNIE MANDELA HAKUNA BIFU
Juzi ndani ya Uwanja wa FNB uliopo Mtaa wa Soccer City nchini humo wakati wa zoezi la kumuaga marehemu Mandela, kivutio kikubwa kilikuwa kwa wanawake wawili waliowahi kuwa na uhusiano na kiongozi huyo.
Winnie Medekizela Mandela, aliyewahi kuwa mke wa Mandela mpaka kutoka kifungoni na Graca Machel aliyekuwa mke mpaka kifo cha Mandela, walitazamwa na waombolezaji wengi kufuatia historia zao kutokuwa na migongano.
Wawili hao, mara kadhaa wamewahi kupiga picha ya pamoja na mzee huyo wakiwa na nyuso za furaha huku wote wakiwa wamemkumbatia.
Viongozi mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete (wa nne mstari wa pili kulia kutoka juu) na mkewe Mama Salma wakifuatilia ibada ya kumbukumbu ya Nelson Mandela.
OBAMA AHUTUBIA NDANI YA JUKWAA LENYE VIOO VYA KUKINGA RISASI
Akitoa hotuba yake kwa wananchi wa Sauzi na waombolezaji wengine duniani kote, Rais wa Marekani, Barack Obama alionekana ndani ya jukwaa lenye vioo visivyoweza kupitwa na risasi (bullet proof).
DUNIA YAANDIKA HISTORIA MPYA
Kuwepo kwa Rais wa Marekani, Barack Obama na Rais wa China, Xi-Jinping kunasemekana ni kuandikwa kwa historia mpya ya dunia kwani viongozi hao hawajawahi kukutana nje ya nchi zao.
Kingine kilichoonekana ni kuandikwa kwa historia mpya ya dunia ni tukio hilo kuwa la kwanza kukutanisha viongozi wazito wa duniani kwa wakati mmoja.
Inadaiwa hata wanaokwenda kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa hawakufikia uzito wa kwenye msiba wa Mandela.
Marais mbalimbali wakiambatana na ujumbe mzito kutoka katika nchi zao walihudhuria msiba huo, ukiachana na watu wengine maarufu na viongozi wa kawaida.
JINA LA KIKWETE LAWA LA KWANZA KWENYE ORODHA
Katika hali iliyoonesha mshikamano kati ya Afrika Kusini na Tanzania, jina la Rais Jakaya Kikwete lilikuwa la kwanza katika orodha ya marais waliokuwa kwenye mwaliko.
Jambo hilo limeongeza hamasa na uhusika wa moja kwa moja kwa Watanzania juu ya msiba huo kutokana na umoja, ushirikiano na kuaminiana kulikooneshwa na Sauzi.
Juzi, Jumatatu, Desemba 9, mwaka huu katika sherehe za Miaka 52 ya Uhuru, zilizofanyika kitaifa, Uwanja wa Uhuru, Dar, Rais Kikwete alizungumzia namna marehemu Mandela alivyoipenda Tanzania na uhusiano mwema wa nchi hizi mbili.
Hilo lilijidhihirisha baada ya Sauzi kumweka Rais Kikwete wa kwanza, akiwaongoza marais na viongozi wengine waliohudhuria msiba na shughuli za mazishi ya shujaa huyo.
NAMBA 3 YAWAMALIZA VIGOGO NCHINI HUMO
Pamoja na yote, namba 3 imeonekana kuweka historia ya kipekee nchini humo kwa kuhusika na vifo vya viongozi wake wakuu.
Mpigania haki mwingine mkongwe, Oliver Tambo aliyezaliwa Oktoba 27, 1917 naye alifariki mwaka 1993 (Aprili 24). Walter Sisulu, alikuwa mpigania uhuru sambamba na Tambo na Mandela, naye alifariki dunia mwaka 2003 (Mei 5, alizaliwa Mei 18, 1912).
Kifo cha Mandela kilichotokea Desemba 5, 2013 kinazidi kutia shaka katika orodha ya namba 3 kila baada ya miaka 10.
Marehemu Nelson Mandela ambaye zoezi la kuuaga mwili wake linakamilika leo kwenye uwanja huo, atazikwa Jumapili ijayo. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi - Amina.Love to hear what you think!